IQNA

Mkutano wa kimataifa wa "Ashura na Kutazamwa Upya Mifumo ya Kuhuisha Tukio la Karbala."

10:59 - January 31, 2009
Habari ID: 1737759
Mkutano wa kimataifa wa "Ashura na Kutazamwa Upya Mifumo ya Kuhuisha Tukio la Karbala" umeanza mjini Beirut Lebanon ukihudhuriwa na shakhsia mashuhuri wa kidini kutoka nchi mbalimbali.
Mwandishi wa IQNA nchini Lebanon ameripoti kuwa mkutano huo unaosimamiwa na Allamah Muhammad Hussein Fadhlullah, marjaa wa Waislamu nchini humo, na Taasisi ya Fikra za Kisasa za Kiislamu unahudhuriwa na wanafikra kutoka Saudi Arabia, Iraq, Iran, Bahrain na Lebanon.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Fikra za Kisasa za Kiislamu Najiib Nuruddin amesema kuwa ajenda kuu ya mkutano huo ni kuchunguza mbinu za kuhuisha kwa njia sahihi tukio la Ashura, suna na ada zinazofanywa kuhusiana na tukio hilo, vyanzo vya kuaminika vya Ashura na mambo yasiyokuwa na uhusiano wa aina yoyote na tukio hilo kubwa.
Nuruddin ameongeza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuchunguza njia za kulipa tukio la Karbala sura ya kibinadamu kwa kuliondoa katika duara finyu la mnasaba wa kidini na kulifanya tukio la kihistoria linalowahusu wanadamu wote.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Fikra za Kisasa za Kiislamu ameashiria hotuba iliyotolewa na Ayatullah Fadhlullah katika mkutano huo na ukosoaji wake wa njia zisizokuwa sahihi zinazotumiwa katika kuhuisha tukio la Ashura ambazo zinachafua sura safi ya Uislamu na madhehebu ya Shia na akasisitiza kwamba: Washiriki katika mkutano huo wametoa wito wa kutazamwa upya suna na ada za Ashura na kueleza tukio la mapinduzi ya Imam Hussein (as) kwa njia sahihi.
Mkutano huo pia unahudhuriwa na malenga na watengezaji filamu na michezo ya kuigiza ambao wanajadili suala la kubainisha tukio la Ashura kwa kutumia fani za sanaa na fasihi. 356365
captcha