IQNA

Al-Azhar yakosoa fatuwa mbovu za mamufti wa Saudi Arabia kuhusiana na Gaza

11:30 - January 31, 2009
Habari ID: 1737912
Harakati ya Maulamaa wa al-Azhar imetoa taarifa ikilaani na kukosoa vikali fatuwa iliyotolewa hivi karibuni na baadhi ya mamufti wa Saudi Arabia ya kukosoa maandamano na mikusanyiko ya kulaani jinai za utawala haramu wa Israel na uungaji mkono kwa watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Maulamaa hao wa Misri wamesema kuwa fatuwa hiyo ya mamufti wa Kiwahabi wa Saudi Arabia ni udhalili mkubwa na hatua isiyo ya kibinadamu.
Kuhusiana na suala hilo, Yahya Ismail, Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Maualamaa wa Misri amesema kuwa maandamano na mikusanyiko hiyo ya kulaani hujuma ya kinyama ya utawala wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza na hasa wanawake na watoto, ni ishara ya wazi ya muamko wa umma wa Kiislamu, alama ya mfungamano na Waislamu wanaokandamizwa katika Ukanda wa Gaza na kizuizi cha kukaririwa hatua za kujipanua utawala wa Israel katika ardhi za Wapalestina pamoja na kuzuia mauaji ya umati ya utawala huo dhidi yao.
Akiashiria hatua ya mamufti hao wa Kiwahabi ya kukwepa kutoa fatuwa ya kuharamisha na kususiwa bidhaa za nchi za Magharibi, Ismail Yahya amesema kuwa, mapambano dhidi ya unyama na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia hayahusiani tu na silaha, bali yanahusu pia bidhaa za Marekani na nchi nyinginezo za Magharibi, ambao ndio waungaji mkono na wadhamini wakuu wa silaha za kisasa zinazotumiwa na utawala wa Israel kuwaua kwa umati Wapalestina, na hasa wale wanoishi katika Ukanda wa Gaza. Amesema, ususiaji huo una nafasi muhimu katika kutoa mashinikizo dhidi ya maghasibu wa Kizayuni. Ismail Yahya ametaka kukatwa kwa uhusiano wote wa kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia wa nchi za Kiarabu na utawala huo.
Ni muhimu kuashiria hapa kwamba, Swaleh al-Haidan, Mkuu wa Baraza Kuu la Makadhi wa Saudi Arabia na baadhi ya mamufti wenye misimamo ya kupindukia mipaka wa Kiwahabi wa nchi hiyo walitoa fatuwa wakiharamisha maandamano na mikusanyiko ya hadhara dhidi ya utawala wa Israel na kupinga kutolewa kwa aina yoyote ile ya fatuwa inayoharamisha ununuzi wa bidhaa za Marekani na Israel katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu. 356340
captcha