IQNA

Kamati ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Israel Gaza inapasa kuundwa

15:56 - February 03, 2009
Habari ID: 1737914
Likichambua masuala ya hivi karibuni ya Ukanda wa Gaza, gazeti la Humanity la nchini Ufaransa limeandika kuwa, kuna udharura mkubwa wa kubuniwa kamati ya kimataifa kwa ajili ya kuchunguza jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza, na kuwafahamisha walimwengu athari za jinai hizo.
Gazeti hilo linasisitiza kwamba, watawala na makamanda wa kijeshi wa jeshi la utawala huo wanapasa kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kujibu mashtaka ya jinai walizotenda dhidi ya raia wasio na hatia huko Gaza.
Gazeti hilo linaendelea kusema kuwa, usitishaji vita wa upande mmoja uliotangazwa na Israel dhidi ya wakazi wa ukanda huo sio dhamana ya kutosha ya kutokaririwa tena mauaji ya umati ya utawala huo dhidi ya wakazi wasio na hatia wa ukanda Gaza, bali watawala wa utawala huo wanapasa kuruhusu kuundwa kwa taifa huru la Palestina litakalokuwa na mji mkuu wake huko Baitul Muqaddas.
Uchambuzi wa gazeti la Humanity unaendelea kusema kuwa, kwa kuendelea kuwaua kwa umati Wapalestina wasio na hatia, kuwashambulia mara kwa mara, kuzusha migawanyiko miongoni mwa makundi ya Kipalestina na kutekeleza operesheni za kijeshi katika ardhi zao, utawala wa Israel umewapokonya kabisa Wapalestina hao utulivu wao wa maisha.
Kuwekwa askari wa kimataifa katika mpaka wa Gaza, kuimarishwa mazungumzo ya kutatua kiuadilifu hitilafu kati ya Wapalestina na Wazayuni na kurejeshwa amani ya kudumu katika eneo zima la Mashariki ya Kati ni mambo mengine ambayo yamechambuliwa kwa kina na gazeti hilo katika toleo lake la hivi karibuni. 356362
captcha