Wataalamu wa masuala ya sheria kutoka nchi za Ulaya na Kiarabu walikutana siku ya Ijumaa huko Paris nchini Ufaransa na kutia saini hati ya kutengeneza filamu ya matukio ya kweli ,documentary, kuhusiana na jinai zilizotekelezwa hivi karibuni na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko katika Ukanda wa Gaza.
Pande mbili hizo zimekubaliana kubuni kamati maalumu ya kitaalamu itakayokusanya nyaraka na ushahidi wa kutosha kuhusiana na jinai hizo zilizotekelezwa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi na hasa wanawake na watoto katika ukanda huo.
Vilevile kwa mujibu wa hati hiyo ya maelewano, jinai zote za Wazayuni zilizotekelezwa katika kipindi cha siku 22 za hujuma ya kinyama ya utawala huo dhidi ya watu wasio na hatia wakiwemo wazee, zitatengenezewa filamu ya matukio ya kweli na kisha kusambazwa ulimwenguni ili kuwafahamisha jinai zilizotekelezwa na utawala huo katika ukanda huo.
Katika kikao cha pamoja kilichofanyika kati ya wanasheria hao, njia za kufuatiliwa kisheria na kufikishwa watawala na makamanda wa jeshi la utawala wa Israel waliohusika na jinai hizo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) pia zilichunguzwa. Wanasheria hao walilaani vikali jinai hizo za kuuawa kinyama watu wasio na hatia na utawala wa Israel.
Ali Khashan, Waziri wa Sheria wa Palestina amesema kuwa, wawakilishi wa zaidi ya jumuiya na mashirika 100 ya sheria ya nchi za Ulaya na Kiarabu walikutana na mjini Paris na hatimaye kutoa taarifa ya kusisitiza azma yao ya kutengeneza filamu iliyotajwa ya jinai za Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza kwa kutegemea ushahidi wa kuaminika. 356653