IQNA

Kikao cha kimataifa cha 'njia za kurekebisha sura ya Uislamu katika nchi za Magharibi' chafanyika nchini Kuwait

11:41 - February 02, 2009
Habari ID: 1738761
Kikao cha kimataifa cha kuchunguza 'njia za kurekebisha sura ya Uislamu katika nchi za Magharibi' kilifanyika siku ya Jumamosi huko Kuwait kwa udhamini wa Baraza la Kimataifa la Fiqhi ya Kiislamu na kwa usimamizi wa Sheikh Nassir Muhammad Ahmad as- Swabah, Waziri Mkuu wa Kuwait.
Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la al-Qabas, Ayatullah Sayyid Abul Qassim Dibaji, Katibu Mkuu wa Baraza hilo amesema katika kikao hicho kwamba, jamii za Waislamu waliowachache na mashirika ya kimataifa ya Kiislamu yana jukumu zito la kuboresha sura ya Uislamu na Waislamu katika nchi za Magharibi. Ametoa ripoti fupi kuhusiana na shughuli za baraza hilo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kusema kuwa ni pamoja na kupunguza hitilafu zilizopo kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu, kuboresha na kudhihirisha sura halisi ya Uislamu kwa wasiokuwa Waislamu, kuimarisha misingi ya kidini na kupambana na watu wenye misimamo mikali na ya kupindukia mipaka katika dini.
Katika kikao hicho, Sheikh Muhammad Asiran, Mufti wa Mji wa Saida (Sidon) nchini Lebanon amesema kuwa watu wenye misimamo mikali na ya kibaguzi katika nchi za Magharibi daima hutuhumu na kujaribu kuwahusisha Waislamu na ugaidi na wakati huohuo kuvitumia vyombo vyao vya habari kutekeleza njama zilizopangwa vyema kwa ajili ya kuharibu jina la Uislamu ulimwenguni.
Huku akisisitiza kwamba dini zote za mbinguni zinamtakia mwanadamu saada humu duniani na huko Akhera, Sheikh Muhammad Asiran amesisitiza kwamba kupambana na misimamo mikali na utumiaji mabavu pamoja na kuimarisha mazungumzo kati ya tamaduni na staarabu mbalimbali, ndiyo njia bora zaidi ya kuleta amani na utulivu duniani.
Sheikh Ibrahim an-Nasirawi, hatibu mashuhuri wa Kuwait ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Kimataifa la Fiqhi ya Kiislamu amesema kuwa fiqhi ina nafasi muhimu katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ya Waislamu.
Baraza hilo linalowajumuisha wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kutoka kila pembe ya dunia, lilibuniwa mwaka uliopita wa 2008 mjini Paris Ufaransa ambapo Ayatullah Sayyid Abul Qassim Dibaji alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wake. 357392
captcha