Kwa mujibu wa gazeti la al sharq al Ausat Mkuu wa Chuo cha Al Azhar Sheikh Muhammad Sayyid Tantawi Februari Mosi alikutana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana la Uingereza Rowan Williams mjini London na wamejadili njia za kupambana na fikra potofu ambazo zinahimiza utumiaji mabavu na siasa kali duniani. Baada ya mazungumzo yao, wametia saini mapatanao ya kupambana na fikra hizo potofu.
Katika mazungumzo hayo na Askofu Mkuu Rowan Williams, Sheikh Sayyid Tantawi ameonya kuhusu kufungamanisha ugadi na dini hasa dini ipendayo amani na ubinadamu ya Kiislamu. Vile vile amekanusha kuwepo hitilafu na fitina za kidini kati ya Waislamu na Wakristo wa Misri.
“Waislamu na Wakristo wa Misri wana haki sawa na ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinapanga njama za kuzusha fitina na mifarakano kati ya wafuasi wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini Misri”, amesema Sheikh Tantawi.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar amesema, dini ya Kiislamu inapinga chuki dhidi ya wafuasi wa dini nyinginezo na kuongeza kuwa mafunzo ya Kiislamu yanasisitiza kuhusu mapambano dhidi ya uzushaji hitilafu, ubaguzi wa rangi, utumiaji mabavu na misimamo ya kufurutu mipaka.
Mwanachuoni huyo wa Misri ametoa wito kwa serikali ya Cairo kufanya jitihada za kuhakikisha watu wa Palestina wanapewa haki zao kisheria. Aidha ameitaka serikali ya London kuushinikiza utawala wa Israel kusitisha jinai zake za kinyama dhidi ya Wapalestina hasa waishio Gaza.
Vile vile amewataka wakuu wa Uingereza kuwashurutisha watawala wa Kizayuni kusitisha hatua zao za kuharibu misikiti ya Palestina na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu kunakofanywa mara kwa mara na Wazayuni.
Kwa upande wake, askofu mkuu wa kanisa la Anglikana la Uingereza Rowan Williams amekishukuru chuo cha al Azhar kwa jitihada zake za kuanzisha mazungumzo baina ya dini na tamaduni mbalimbali na uhimazaji wake wa thamani za maelewano duniani. 357569