IQNA

Rais wa Ireland: Dharau ya Wamagharibi kwa Qur'ani ni jambo la kusikitisha

10:08 - February 04, 2009
Habari ID: 1740020
Akitembelea kituo cha Qur'ani cha Beit al-Qur'an huko mjini Manama mji mkuu wa Bahrain, Rais Mary McAleese wa Ireland amesema kuwa maana na mafundisho ya Qur'ani tukufu yanahubiri amani na kuishi pamoja wanadamu kwa amani na kwamba hatua ya watu wenye misimamo ya kupindukia katika nchi za Magharibi ya kukidharau kitabu hicho kitakatifu ni jambo la kusikitisha mno.
Kwa mujibu wa gazeti la Bahrain la Ar-Rayah, Rais Mary McAleese ameyasema hayo alipokitembelea kituo kilichotajwa na kujionea mwenyewe athari na nyaraka za pekee na za aina yake za Qur'ani zilizoandikwa kwa mkono zinazohifadhiwa katika kituo hicho. Amesema, nyaraka hizo zinathibitisha utukufu na thamani kubwa ya utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu katika zama tofauti pamoja na umuhimu unaotolewa na watu wa Bahrain kwa urithi wa ustaarabu wa Kiislamu.
Abdul Latif Jassim Kano, muasisi wa kituo hicho alimfafanulia Rais wa Ireland masuala mbalimbali kuhusiana na jumba la mambo ya kale, maktaba, msikiti, sanaa za Kiislamu, nyaraka zilizoandikwa kwa mkono za Qur'ani na Kiislamu pamoja na ukumbi wa mikutano wa Muhammad bin Khalifa Aal Khalifa wa kituo hicho.
Amesema, lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kuwafahamisha walimwengu urithi wenye thamani kubwa wa utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu pamoja na kuhifadhi huko nyaraka za kale za Kiislamu zilioandikwa kwa mkono.
Mwishoni mwa matembezi ya Rais wa Ireland katika kituo hicho, Abdullatif Jassim Kano alimkabidhi vitabu na zawadi nyinginezo za ukumbusho wa safari yake katika kituo hicho. 358679
captcha