Kituo cha Kishia cha al-Qaim cha nchini Ubelgiji kimetoa taarifa kikibainisha wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na vikwazo na mashinikizo, yakiwemo ya kutiwa nguvuni shakhsia na wasomi wa Kishia, yanayotekelezwa na serikali ya Bahrain dhidi ya shughuli za Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la As'watul Iraq, taarifa ya kituo hicho cha Kiislamu inasema kuwa, matukio ya kisiasa ya hivi karibuni nchini Bahrain, ikiwa ni pamoja na kutiwa mbaroni kwa wanazuoni na wasomi wa Kishia nchini humo, ni jambo la kusikitisha mno na kwamba huenda likazidisha mivutano na ghasia za kimadhehebu nchini. Taarifa hiyo imewataka viongozi wa Bahrain kuwaachilia huru mara moja watu waliotiwa nguvu na kufanya marekebisho ya kisiasa na kijamii nchini humo kwa maslahi ya raia wake wote na bila ya ubaguzi.
Taarifa hiyo imesema kwamba, ubaguzi dhidi ya Mashia unaofanywa na viongozi wa Bahrain, kutopewa nafasi sawa za kisiasa, kiuchumi na kijamii pamoja na kubanwa katika utekelezaji wa shughuli zao za kimadhehebu na kiibada ni miongoni mwa matatizo yanayowakumba Mashia wa nchi hiyo.
Wiki iliyopita, askari usalama wa Bahrain waliwatia nguvuni, Hassan Mushaima, Imam wa Msikiti wa Imam Swadiq (as) ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Uhuru na Demokrasia cha Bahrain, Sheikh Muhammad Habib al-Miqdad, Katibu Mkuu wa Taasisi ya az-Zahra (as) na Abdul Jalil as-Sinkis, Mkuu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Bahrain ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Manama pamoja na idadi kadhaa ya raia wa Kishia wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kulalamikia katiba ya nchi hiyo pamoja na kutoa hotuba za kichochezi dhidi ya serikali ya Manama. 358709