Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amemtumia ujumbe Ekmeleddin Ihsanoghlu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, akisema kuwa nchi hiyo iko tayari kushirikiana na nchi za Kiislamu kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa Ukanda wa Gaza na kuimarisha amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa OIC, Waziri Lavrov amesisitiza katika ujumbe wake kwamba, Russia imefanya mashauriano ya ushirikiano na makundi na vyama kutoka pande mbalimbali za dunia na hasa nchi za Kiislamu katika Mashariki ya Kati kwa ajili ya kumaliza mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza na kwamba tayari imetuma shehena nyingi za misaada na madaktari kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa mashambulio hayo ya utawala haramu wa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria mipango ya kufanyika mkutano wa kimataifa kwa ajili ya amani ya Mashariki ya Kati huko Moscow mwaka huu na kuongeza kuwa kukomeshwa kwa jinai za Gaza, kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu na kufunguliwa kwa vivuko vya Gaza ni malengo makuu yanayofuatiliwa na serikali ya Moscow.
Lavrov amezitaka nchi za Kiislamu ziwe na imani kwamba malengo hayo yatafikiwa. 361432