Mkutano wa kimataifa wa "Kusasisha Fikra za Kiislamu, Udharura, Malengo na Mipaka yake" umenza kazi zake katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa. Mkutano huo utaendelea kwa kipindi cha siku tano.
Kituo cha habari cha Sabanet kimeripoti kuwa mkutano huo wa kimataifa unasimamiwa na Jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Kiislamu kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Sanaa na Iman vya Yemen.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Kiislamu Ja'far Abdulsalam amesema kuwa miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kuainisha stratijia kamili ya mpango wa kusasisha fikra za Kiislamu, kuchunguza nafasi ya vyuo vikuu na taasisi za kielimu katika kulinda stratijia hiyo, kubainisha Uislamu kama dini ya ulimwengu mzima na ya zama na mahala pote na kuthibitisha kwamba mpango wa kusasisha fikra za Kiislamu ni faradhi ya kidini.
Ameongeza kuwa wanafikra na wasomi wanaoshiriki katika mkutano huo wanachunguza pia mirengo mbalimbali ya kuhuisha fikra za Kiislamu, kanuni zake muhimu na wajibu wa vyuo vikuu vya Kiislamu katika kutayarisha ulimwengu wa Kiislamu ili ukubali ijtihadi na fikra mpya katika masuala ya kidini na kisheria. 362210