Washiriki katika kongamano la kimataifa la "Vyombo vya Habari, Uhuru wa Kusema na Kuzivunjia Heshima Dini" katika mji wa Sanaa nchini Yemen wamesisitiza juu ya udharura wa kuundwa kamati ya waandishi, wanahabari, wataalamu wa fiqhi na wanafikra wa Kiislamu kwa ajili ya kubuni mkakati wa kupambana na mwenendo wa kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu.
Taarifa iliyotolewa jana mwishoni mwa mkutano huo imetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu sababu za kuvunjiwa heshina Uislamu na propaganda chafu za kuwafanya Wamagharibi wauogope Uislamu. Taarifa hiyo imesema;"Uhasama dhidi ya Waislamu na dini yao ni kinyume na sheria na kanuni za kimataifa."
Taarifa hiyo pia imesisitiza juu ya udharura wa kuwepo mawasiliano ya daima kati ya taasisi za upashaji habari na za kiutamaduni za nchi za Kiislamu kwa ajili ya kulinda thamani za dini hiyo, kuwaelimisha wasiokuwa Waislamu misingi na mafundisho ya dini hiyo tukufu, kujibu maswali na tuhuma zisizokuwa sahihi zinazotolewa dhidi ya dini ya Kiislamu na kusahihisha taswira isiyokuwa sahihi ya Wamagharibi kuhusu Uislamu na Waislamu.
Washiriki katika mkutano wa Yemen pia wamevitaka vyuo vikuu vya nchi za Kiislamu kufanya utafiti kamili na wenye malengo maalumu kwa ajili ya kuimarisha mazungumzo kati ya dini mbalimbali na kutoa majibu kwa hujuma za kipropaganda za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Wanafikra na wataalamu wa vyombo vya habari walioshiriki katika mkutano huo pia wamesisitiza juu ya umuhimu wa kuanzishwa kituo cha kimataifa cha ulinganiaji wa Kiislamu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa nguvu kazi ya wataalamu, kueneza utamaduni sahihi wa Kiislamu na kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani wa dini hiyo. Imeitaka Jumuiya ya kimataifa ya Ulimwengu wa Kiislamu kuchunguza suala la kuasisi kituo hicho katika mkutano wa pili wa kimataifa wa "Vyombo vya Habari na Uhuru wa Kusema" utakaofanyika nchini Indonesia. 362201