Gazeti la al-Bayaan la Qatar limesema kuwa, duru hiyo ya mafunzo imeandaliwa na Taasisi ya Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume (saw) ya mjini Sharjah. Mafunzo hayo ambayo yanawashirikisha wahubiri wa Kiislamu wapatao 130 kutoka nchi mbalimbali zisizo za Kiislamu na hasa kutoka nchi za Magharibi, yataendelea kwa muda wa wiki mbili.
Ibrahim al-Hammadi, Mkuu wa taasisi iliyotajwa katika eneo la mashariki mwa Sharjah amesema kuhusiana na suala hilo kuwa, Ahmad al-Qadhaa, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mafundisho ya Qur'ani na Utafiti wa Kiislamu cha Dubai ndiye atakayetoa mafunzo hayo ya Qur'ani katika kipindi hicho. Ameongeza kuwa, masomo hayo yanatolewa katika fremu ya taasisi hiyo kuzingatia mafunzo ya sheria za Kiislamu na hasa mafunzo yanayohusiana na Qur'ani na kunyanyua kiwango cha elimu ya wahubiri wa Kiislamu katika nchi tofauti.
Ibrahim al-Hammadi amesema kuwa katika masomo hayo utangulizi wa misingi ya tajweed, usomaji na istilahi mbalimbali za elimu ya tajweed utachunguzwa. Amesema, washiriki katika kozi hiyo watafunzwa sheria na kanuni zote za usomaji wa Qur'ani kwa kutumia mbinu ya tajweed. 362561