IQNA

Rabat, mwenyeji wa kikao cha 'Israel: Jinai za Vita na Mauaji ya Umati'

12:40 - February 14, 2009
Habari ID: 1743620
Kikao cha 'Israel: Jinai za Vita na Mauaji ya Umati' ambacho kimeandaliwa na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa nchi za Kiislamu, ISESCO na kwa ushirikiano wa jumuiya za Palestina pamoja na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, kimeanza leo Jumamosi katika makao ya shirika hilo huko Rabat nchini Morocco. Kikao hicho kitaendelea hadi kesho Jumapili.
Kwa mujibu wa ISESCO, wawakilishi wengi wa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, wataalamu mashuhuri wa kimataifa wa masuala ya sheria, mawakili wa kimataifa na pia idadi kubwa ya mashahidi walioshuhudia jinai za utawala haramu wa Israel zikitekelezwa dhidi ya watu wasio na hatia wala ulinzi katika Ukanda wa Gaza wanashiriki katika kikao hicho cha kimataifa.
Washiriki watachunguza jinai zilizotekelezwa dhidi ya wakazi wasio na ulinzi wa Gaza na kisha kuwasilisha ushahidi wa kuaminika wa mauaji ya umati dhidi ya wakazi hao yaliyotekelezwa na utawala wa kibaguzi wa Israel. Washiriki vilevile watatafuta njia zinazofaa kwa ajili ya kutetea haki za wananchi madhlumu wa Palestina na pia kufanya juhudi za kufikishwa wahusika wa mauaji hayo ya umati ya Ukanda wa Gaza mbele ya mahakama zenye itibari za kimataifa. Washiriki wa kikao hicho cha Rabat wana lengo la kukusanya nyaraka zote za kuaminika za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya umati yaliyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza na kuziwasilisha katika mahakama za kimataifa ili kufuatiliwa kisheria watawala wote wa kijeshi na kisiasa wa Israel waliohusika na jinai hizo dhidi ya binadamu.
Nyaraka za madaktari wa Ulaya waliofanikiwa kuingia katika Ukanda wa Gaza wakati wa kutekelezwa jinai hizo pia zitategemewa kuhusiana na suala hilo.
Abdul Aziz Othman at-Tuwaijri, Katibu Mkuu wa ISESCO ameshiria umuhimu wa kufanyika kikao hicho katika hotuba yake ya ufunguzi na kugusia umuhimu wa kutatuliwa mgogoro wa Palestina na changamoto zinazoikabili jamii ya kimataifa katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wasio na ulinzi wa Palestina. 363364
captcha