Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Morocco, mkutano huo ambao umeandaliwa na Jumuiya ya al-Muhammadiyya ya maualama wa nchi hiyo unafanyika pambizoni mwa maonyesho ya kimataifa ya vitabu katika mji wa Casablanca.
Nur ad-Deen Miladi, mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Masuala ya Kiarabu na Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Nuret Hamilton cha nchini Uingereza na wataalamu pamoja na wasomi wengine wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu wanashiriki katika mkutano huo wa siku mbili.
Picha zinazotolewa na vyombo vya habari na hasa vya nchi za Magharibi kuhusiana na Uislamu na Waislamu pamoja na iwapo kweli vyombo hivyo vinatoa picha halisi kuhusiana na Uislamu, ni mambo yanayojadiliwa na kupewa uzito na washiriki wa mkutano huo.
Jumuiya ya al-Muhammadiyya ya wanazuoni wa Morocco imetoa taarifa ikisema kuwa, kufuatia matukio ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi daima vimekuwa vikifanya propaganda chafu na kutoa madai yasiyo na msingi wowote kwa ajili ya kuuhusisha Uislamu na ugaidi. Taarifa hiyo imeendelea kusema, daima vyombo hivyo vyenye chuki dhidi ya Uislamu vimekuwa vikitoa sura potofu na yenye madhara kwa Uislamu kwa kudai kwamba Waislamu na Waarabu ni chanzo cha shari na mabaya yote duniani, jambo ambalo imesisitiza kwamba ni hatari kubwa kwa usalama wa dunia.
Taarifa hiyo imeendelea kusema, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2007 na taasisi mbalimbali za utafiti wa kimataifa, asilimia 80 ya habari za vyombo vya habari vya Magharibi, kuhusiana na Uislamu na Waislamu hupotoshwa kwa makusudi ili kuzusha hofu dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hiyo tukufu.
Jumuiya ya al-Muhammadia ya wanazuoni wa Morocco imelitaja suala hilo kuwa linatia wasiwasi mkubwa na kuwataka wamiliki wa vyombo vya habari katika ulimwengu wa Kiislamu kubuni njia madhubuti za kutoa habari sahihi kuhusiana na Uislamu na Waislamu kwa walimwengu, na vilevile kukabiliana na hujuma hiyo ya kiuadui ya vyombo vya habari vya nchi za Magahribi. 363820