IQNA

Utawala wa Israel waharibu urithi wa kielimu na kiutamaduni wa Palestina

14:29 - February 16, 2009
Habari ID: 1744668
Katika kipindi cha vita vyake vya kichokozi vya siku 22 dhidi ya watu wasio na hatia huko katika Ukanda wa Gaza, jeshi la utawala huo lililenga kwa makusudi vituo vya kielimu na kiutamaduni vya Wapalestina zikiwemo shule, vyuo vikuu na taasisi za kielimu na kiutamaduni kwa lengo la kuharibu urithi wa utamaduni wa Wapalestina.
Hayo yamesemwa na Abdul Adhim al-Maghribi, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mawakili wa Kiarabu katika kikao kilichofanyika mjini Rabat Morocco chini ya anwani 'Israel: Jinai za Kivita na Mauaji ya Umati'.
Amesema, sheria za kimataifa zinatambua na kusisitiza juu ya haki ya mapambano ya wananchi wa Palestina katika kupigania kujitawala kwa nchi yao na pia kuunda serikali huru katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na maghasibu wa Israel. Ameongeza kuwa, mashirika na jumuiya za kimataifa zinaweza kufanya utafiti na uhakiki kuhusiana na jinai zilizofanywa hivi karibuni na utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Palestina huko katika Ukanda wa Gaza na kisha kuuwasilisha katika mahakama za kimataifa zinazofuatilia jinai za kivita.
Al-Maghribi amemtamka Luis Moreno Ocampo, Mwendeshamashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutekeleza vyema majukumu yao kwa kuwafautilia kisheria watawala wa kisiasa na kijeshi wa utawala haramu wa Israel waliohusika na jinai hizo, kuvunja sheria za kimataifa na kukiuka wazi haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza.
Adnan Abu Hasana, msemaji wa kitengo cha habari-maelezo cha shirika linalowashughulikia wakimbizi wa Palestina UNRWA ni miongoni mwa watu waliozungumza katika kikao hicho cha Rabat ambapo amezungumzia juhudi zinazofanywa na mashirika pamoja na taasisi za kimataifa za masuala ya sheria kwa lengo la kukusanya nyaraka za kutosha za kuwafikisha watawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusiana na jinai hizo za Gaza.
Kikao hicho cha Rabat kimeandaliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (ISESCO) kwa ushirikiano wa makundi ya mapambano ya Palestina. 364631
captcha