Mauaji mengine ya kinyama ya hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa mauaji kama hayo ambayo yamekuwa yakitekelezwa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia ni yale ya siku 22 yaliyofanywa katika Ukanda wa Gaza, ambapo jeshi la utawala haramu wa Israel liliwachinja kinyama Wapalestina wapatao 1300 wakiwemo wanawake na watoto.
Akizungumzia suala hilo katika kikao maalumu kilichoandaliwa huko Rabat Morocco, kuzungumzia jinai zilizotekelezwa hivi karibuni na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wakazi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza, Abdul Aziz bin Othman al-Tuwaijri, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (ISESCO) amesema kwamba, inasikitisha kushuhudia kwamba jinai na mauaji hayo ya umati yametekelezwa na Wazayuni huku jamii ya kimatifa ikiwa imenyamaza kimya, licha ya kuwa mauaji hayo yalikuwa mabaya na ya kinyama zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia wala ulinzi katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
al Tuwaijri amesema, tokea wakati wa kubuniwa utawala haramu wa Israel mwaka 1948 hadi leo, utawala huo umekuwa ukikiuka wazi sheria za kimataifa na haki za binadamu kwa kuwaua kinyama Wapalestina wasio na hatia katika ardhi zao unazozikalia kwa mabavu. Huku akisisitiza kwamba miongoni mwa majukumu ya ISESCO ni kuchangia juhudi za kupatikana amani, uthabiti na amani duniani kupitia elimu, sayansi na utamaduni, al-Tuwaijri ameelezea matumaini yake kwamba kikao hicho cha Rabat ni hatua ya mwanzo katika mwenendo wa kuhukumiwa katika mahakama za kimataifa watawala wa kisiasa na kijeshi wa utawala haramu wa Israel waliohusika na jinai dhidi ya binadamu huko katika Ukanda wa Gaza.
Amesema kuwa, mapendekezo ya kikao cha Rabat yatawasilishwa katika kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu huko Kuwait ili kujadiliwa na kuchukuliwa hatua za lazima.
Washiriki wa kikao hicho ambao wamekuwa ni pamoja na wawakilishi wa mashirika na taasisi muhimu za kimataifa za masuala ya sheria, wamekubaliana kukusanya nyaraka na ushahidi wa kutosha wa kuwawezesha kuwashtaki watawala wa Isreal katika mahakama husika za kimataifa kutokana na jinai zao dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza. 364403