Arsalan Qarjal, mwanachama wa Barala la Waislamu la Uholanzi na mtafiti na mhadhiri wa Kiislamu katika Chuo Kikuu Huru cha nchi hiyo kilichoko mjini Amsterdam amesema kuwa kuheshimiwa misingi ya Kiislamu pamoja na thamani zake za kiutamaduni ni sharti kuu na muhimu la kufanyika mazungumzo kati ya Waislamu na jamii za nchi za Magharibi.
Akizungumza Jumatatu na gazeti al kimataifa la as-Sharqul Ausat, Qarjal amesema kuwa kuhusishwa misingi na mafundisho ya Kiislamu na baadhi ya tamaduni na mila zisizokuwa na uhusiano wowote na Uislamu, ni jambo linalopelekea kueleweka vibaya Uislamu katika nchi za Magharibi. Amesisitiza juu ya kufanyika mazungumzo halisi yaliyosimama juu ya misingi ya ustaarabu na utamaduni sahihi kati ya Magharibi na ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kibinadamu ulimwenguni.
Amesema kuwa kuenezwa propaganda chafu dhidi ya Uislamu na kutofahamika vyema mafundisho halisi ya Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi, ni jambo ambalo limepelekea kutolewa matusi na dharau dhidi ya dini hii tukufu. Amesema kuhusishwa Uislamu na baadhi ya itikadi na mila potofu na kutoelewa vyema baadhi ya Waislamu mafundisho halisi ya dini yao, kunapelekea pia kueleweka vibaya dini hii tukufu katika nchi za Magharibi na hivyo kuenezwa misimamo na mielekea ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nchi hizo.
Mwanafikra huyo wa Kiislamu amesema, kutangazwa Uislamu sahihi kupitia vyombo vya habari, kuandaliwa vikao na makongamano ya pamoja yanayohudhuriwa na wawakilishi wa dini, kuimarishwa ushirikiano wa taasisi za kiutamaduni na mafunzo kwa ajili ya kufahamika vyema Uislamu halisi, ni miongoni mwa njia zinazopasa kuchukuliwa ili kuondoa picha potofu inayotawala katika nchi za Magharibi kuhusiana na Uislamu. 365235