Baada ya kutembelea makazi yaliyoharibiwa na mashambulizi ya Israel na kuzungumza na waathirika wa unyama huo, Brian Baird amesisitiza kuwa kusikiliza maelezo ya mauaji ya watoto waliokuwa majumbani na shuleni, mauaji ya watu wote wa familia moja na vitendo vya Israel vya kuzuia misaada ya kibinadamu kwa majeruhi vinaumiza mno moyo wa mwanadamu. Amesema, yaliyotukia Gaza na hali inayoendelea kulikumba eneo hilo inatikisa nyoyo na haiwezi kuelezeka kwa maneno.
Brian Baird na Keith Ellison ni wawakilishi wa kwanza wa Bunge la Marekani kutembelea eneo la Ukanda wa Gaza tangu harakati ya Hamas ichukue madaraka katika eneo hilo zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Ellison ambaye ni mwakilishi wa kwanza na pekee Muislamu katika Bunge la Marekani amesema maelezo kuhusu maafa yaliyowapata watoto wadogo wa Gaza yanasikitisha sana. Amekosoa vikali hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu kwa raia wa Gaza na akasisitiza kuwa malori yaliyosheheni misaada ya kibinadamu yamezuiwa kuingia Gaza wakati raia wa eneo hilo hususan wanawake na watoto wadogo, wakihitajia mno chakula, maji na tiba. 366730