Kwa mujibu wa tovuti ya al-Muslim, Ekmeleddin Ihsanoghlu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiislamu amesema katika taarifa hiyo kwamba, lengo hasa la mipango ya utawala wa Israel ni kuharibu kabisa utambulisho wa Kiislamu wa msikiti wa al-Aqsa na kuufanya wa Kiyahudi.
Oghlu amesema, katika kutekeleza mipango hiyo, utawala huo umekuwa ukiwafanya wakazi wa Kipalestina wa mji huo kuwa wakimbizi na kwamba siasa hizo zinahatarisha mustakbali wa msikiti huo mtakatifu. Amesema, matokeo yake ni hatari mno.
Vilevile amesisitiza kwamba siasa hizo hatari za utawala wa Israel ni uchokozi na ukiukaji wa wazi wa Azimio la Nne la Geveva kwa sababu azimio hilo linasisitiza kwamba dola lolote linalokalia kwa mabavu ardhi za taifa jingine, halipasi kuharibu majengo wala kufuta utambulisho wa taifa hilo.
Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Nchi za Kiislamu mwishoni mwa taarifa hiyo amezitaka nchi wanachama wa umoja huo, Jumuiya ya Quds na makundi mengine ya kieneo na kimataifa kutoa radiamali ya haraka kuhusiana na uchokozi huo wa wazi wa Israel katika eneo la Quds Tukufu na kutoa mashinikizo ya kuulazimisha usimamishe mara moja mipango hiyo haribifu katika eneo hilo. 368995