IQNA

Umoja wa Kiislamu njia pekee ya kukabiliana na hukumu ya mahakama ya ICC dhidi ya Rais wa Sudan

16:02 - March 10, 2009
Habari ID: 1754429
Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kutiwa nguvuni Rais Omar al Bashir wa Sudan ni dharau ya wazi kwa serikali na taifa la nchi hiyo, na upinzani dhidi ya dhulma hiyo unahitaji kuwepo umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Hayo yamesema na Imam wa Swala ya Ijumaa wa Piranshahr nchini Iran Sheikh Mustafa Mahmudi. Ameashiria dhulma ya viongozi wa ubeberu dhidi ya Waislamu kote duniani na akasema kuwa Marekani na serikali vibaraka wake zimethibitisha urongo wa madai yao eti ya kutetea haki za binadamu kwa mauaji ya umati dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Sheikh Mustafa Mahmudi amekosoa pia kimya cha nchi za Kiarabu mbele ya jinai hizo na akasema kuwa nchi hizo ambazo zinapaswa kuwatafuta wahalifu halisi yaani viongozi wa utawala wa kigaidi wa Israel, zinatafuta visingizio vingine ili kukwepa majukumu yao.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya Piranshahr amesema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kimsingi iliasisiwa kwa ajili ya kuwatakasa watenda jinai na haistahiki kushughulikia matatizo kama hayo.
Ameongeza kuwa mahakama hiyo imetoa hukumu ya kutiwa mbaroni Rais wa Sudan kwa sababu ya uungaji mkono wake kwa wananchi wa Palestina na imenyamaza kimya mbele ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sheikh Mustafa Mahmudi ameashiria wajibu wa Waislamu wa kufichua jinai na uhalifu wa mabeberu na akasisitiza kuwa njia sahihi ya kukabiliana na ubeberu wa kimataifa ni ushirikiano wa karibu wa nchi za Kiislamu.
Ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni kigezo bora cha mapambano dhidi ya ulimwengu wa Magharibi na akautaka umma wa Kiislamu kuimarisha umoja na mshikamano ili kuweza kukabiliana na mabeberu. 375265
captcha