IQNA

Ahlubaiti wa Mtume (saw), daraja la mawasiliano ya Waislamu

11:11 - March 11, 2009
Habari ID: 1754722
Imam Ali bin Mussa al Ridha na Watu wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (saw) ni rasilimali kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu na daraja la mawasiliano la Waislamu wote.
Hayo yamesemwa na Dakta Rahimi ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kielimu ya Chuo Kikuu Huria cha Mash'had nchini Iran.
Amesema kuwa kuwatukuza na kuwaenzi maimamu kutoka Nyumba ya Mtume amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, kunaunufaisha Uislamu, na kuwakosea heshima ni kudhoofisha Uislamu na Waislamu.
Dakta Rahimi ameashiria nafasi ya haram ya Imam Ali bin Mussa al Ridha ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume na akasema kuwa eneo hilo linaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu kutokana na kuwa kituo muhimu cha kidini. Amesisitiza juu ya udharura wa umoja na mshikamano kati ya makundi yote ya Kiislamu.
Amesema kuwa tatizo letu ni kuwa kuna itikadi zilizoingizwa katika ulimwengu wa Kiislamu ambazo hazina mfungamano au uhusiano wa aina yoyote na dini hiyo na mafundisho yake. Dakta Rahimi amesisitiza kuwa hitilafu zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu zinatokana na mitazamo hiyo iliyoingizwa katika dini.
Amesema kuwa kutokuwepo umoja kati ya Waislamu kumesababisha migogoro mingi kama kukaliwa kwa mabavu Palestina, kubakia nyuma umma wa Kiislamu, uendeshaji mbaya wa masuala mbalimbali ya Waislamu na uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya nchi za Kiislamu. 375977
captcha