Akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano huo Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri amesema kuwa mkutano huo ni hatua kubwa katika kutekeleza thamani za hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzin ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ya kurejesha izza na fahari ya Waislamu.
Ayatullah Taskhiri ameupongeza umma wa Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya maulidi ya Mtume Muhammad (saw) na akasema mahudhurio ya wanafikra, wasomi na maulamaa wa Kiislamu kutoka nchi na mataifa mbalimbali katika Mkutano wa Kimatafa wa Umoja wa Kiislamu ni fursa nzuri ya kuchunguza misingi na thamani zinazowaunganisha Waislamu na kutafakari njia za kukabiliana na njama za kuwatenganisha.
Amesisitiza kuwa mkutano huo utakuwa na kheri nyingi kwa Waislamu na kuwakatisha tamaa maadui wa dini hiyo.
Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri ameashiria masuala na migogoro mbalimbali inayoukumba umma wa Kiislamu hususan mashambulizi ya siku 22 yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na akasema, baadhi ya nchi za Kiislamu hazikuchukua msimamo mzuri wa kuwanusuru wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na Palestina kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa suala hilo linaonyesha kwamba kuna hitilafu kati ya Waislamu na kwa msingi huo maudhui ya Mkutano wa 22 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ni "Umma wa Kiislamu na Mipango ya Kistratijia kwa Ajili ya Kukabiliana na Changamoto za Umoja."
Mkutano wa 22 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulizunduliwa jana Ijumaa mjini Tehran ukihudhuriwa na wanafikra na maulamaa 200 wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani.
377457