IQNA

Muttaki asema katika mazungumzo yake na Mfalme Abdullah:

Mbinu ya maadui wa umma wa Kiislamu ni kuzusha hitilafu na mifarakano

18:24 - March 17, 2009
Habari ID: 1757153
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameunga mkono juhudi zinazofanyika kwa lengo la kuyaunganisha makundi ya Kipalestina na kusuluhisha baina ya nchi za Kiarabu na Kiislamu na akasema kuwa maadui wanatumia mbinu ya kutenganisha na kuzusha fitna kati ya Waislamu na kwa msingi huo zinapaswa kufanyika juhudi za kupambana na njama hizo.
Manouchehr Muttaki ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Mfalme Abdullah bin Abdulaziz wa Saudi Arabia mjini Riyadh.
Amesema kuwa uhusiano wa pande mbili unahitajia harakati mpya na kwamba hali ya sasa ya eneo la Mashariki ya Kati na ya kimataifa inazilazimu nchi mbili za Iran na Saudi Arabia kushauriana na kubadilishana mawazo zaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa katika hali ya sasa maadui wa umma wa Kiislamu wamepata kipigo na kufeli huku umma wa Kiislamu ukipata ushindi katika kukabiliana na maadui hao.
Kwa upande wake Mfalme Abdullah wa Saudia amemtumia salaamu maalumu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais wa Iran na akasema kuwa analipa umuhimu na heshima maalumu taifa na serikali ya Iran. Amesema kuwa taifa la Iran ni taifa kubwa na lenye historia ya siku nyingi na kwamba uhusiano wa Riyadh na Tehran umejengeka juu ya misingi ya itikadi za Kiislamu, ujirani mwema, udugu na urafiki.
Mfalme wa Saudia pia amesisistiza juu ya nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kutetea masuala ya Kiislamu na Kiarabu na ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja mbalimbali. 378337
captcha