Kwa mujibu wa Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Morocco, kikao hicho ambacho kimeandaliwa na wizara hiyo kwa ushirikiano wa Sekretarieti ya Wakfu ya Morocco na pia Benki ya Ustawi ya Kiislamu, kitachunguza zaidi njia za kuimarisha mchango wa wakfu katika ustawi wa nchi za Kiislamu.
Kikao hicho ambacho hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili kitachunguza mitazamo ya wanafikra, wanazuoni na wasomi mbalimbali wa Kiislamu na kisha kuchagua njia bora zaidi ya kuimarisha shughuli za wakfu katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Hii ni mara ya kwanza kwa kikao hicho kufanyika nje ya mipaka ya Kuwait. Morocco imechaguliwa kuwa mwenyeji wa kikao hicho katika hali ambayo imeshindwa kabisa kuandaa vikao vya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu, ambavyo ni muhimu zaidi kuliko vikao vya wakfu, bali pia imeanzisha hujuma kubwa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa kisingizio cha eti kulinda thamani za kidini.
Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo pia yamekuwa yakitoa ripoti kuhusu operesheni kubwa za kiusalama zinazofanywa na polisi ya nchi hiyo dhidi ya watu wanaosemekana kuwa wamekubali ukweli na kufuata fikra za madhehebu ya Ahlul Bait katika miji ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Jumamosi iliyopita pia maafisa wa serikali ya nchi hiyo walifunga shule moja inayoendeshwa na raia wa Iraqi kwa kisingizio kwamba inaeneza fikra za Kishia nchini. Serikali ya nchi hiyo pia hivi karibuni ilichukua hatua ya kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kisingizio hichohicho kisicho na msingi cha kuenezwa Ushia nchini humo. 380209