Sheikh Mustafa Ismail alikuwa qari maarufu na miongoni mwa vinara wa kisasa katika qiraa au usomaji wa Qur’ani nchini Misri. Alijulikana pia kuwa mwanzilishi wa mtindo maalumu wa qiraa uliochanganya nguvu ya uwasilishaji, sauti yenye mvuto na matumizi ya ustadi wa maqamat (mizani ya sauti) kwa namna inayotumikia vyema maana za Qur’ani Tukufu.
Mustafa Ismail alizaliwa tarehe 17 Juni 1905 katika kijiji cha Mayt Ghazal, kilichopo katika mji wa Al‑Santa, mkoa wa Gharbia nchini Misri. Alikulia katika mazingira yaliyosheheni malezi ya Qur’ani, akaihifadhi Qur’ani Tukufu akiwa bado mdogo. Baadaye alijiunga na Taasisi ya Ahmadi huko Tanta kusomea elimu za qiraa na kanuni za tajwidi chini ya usimamizi wa wanazuoni na wasomaji wakubwa.
Vipaji vyake vya kipekee katika usomaji vilidhihirika mapema. Kwa sababu ya sauti yake ya pekee na uwezo wake wa kuvutia katika qiraa, alipata umaarufu mkubwa kote Misri na kuwa miongoni mwa wasomaji mashuhuri wa zama zake. Mwaka 1944, Redio ya Misri ilimteua kuwa msomaji rasmi wa Qur’ani, na pia akachaguliwa kuwa msomaji wa kasri la kifalme wakati wa utawala wa Mfalme Farouk.
Safari yake ya Qur’ani ilisimama juu ya hatua nyingi muhimu. Kwa miaka mingi alisoma Surah Al‑Kahf katika Msikiti wa Al‑Azhar, na qiraa zake zilikuwa zikitangazwa kupitia Redio ya Misri na kufika sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu. Usomaji wake uliendelea kuwa chemchemi ya ilhamu kwa vizazi vya wasomaji na wapenda Qur’ani Tukufu.
Baada ya kusafiri katika nchi nyingi za Kiarabu, Kiislamu na hata nchi za nje, akifikisha ujumbe wa Qur’ani Tukufu katika mabara mbalimbali, Sheikh Mustafa Ismail alitunukiwa lakabu ya “Balozi wa Qur’ani Duniani”. Miongoni mwa matukio ya kihistoria katika maisha yake ni kusoma Qur’ani Tukufu katika Msikiti wa Al‑Aqsa mwaka 1977.
Mustafa Ismail alipata heshima kubwa kutoka kwa mamlaka na pia kutoka kwa wananchi, na alitunukiwa medali na tuzo nyingi za ndani na kimataifa, miongoni mwazo Medali ya Elimu mwaka 1965 na Nishani ya Mwerezi wa Lebanon, pamoja na tuzo nyingine nyingi alizopewa kwa juhudi zake katika kuitumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Ustadh Mustafa Ismail anatambuliwa kuwa ni “madrasah” kamili katika sanaa ya usomaji wa Qur’ani, akitofautishwa na ustadi wake wa hali ya juu katika matumizi ya maqamat za sauti na uwezo wake wa kuzitumia kwa namna inayodhihirisha maana za Qur’ani na kugusa kwa kina nyoyo za wasikilizaji.
Sheikh Mustafa Ismail alifariki dunia tarehe 26 Desemba 1978 baada ya maisha yaliyojaa roho ya ibada na huduma kwa Qur’ani, akiacha urithi mkubwa wa qiraa unaoendelea kugusa nyoyo za Waislamu duniani kote.
Hapa chini mtasikia vipande kutoka baadhi ya qiraa adhimu za Sheikh Mustafa Ismail.
3497904