Mpango huu unatekelezwa kwa mujibu wa maelekezo ya Sheikh wa Al‑Azhar, Dkt. Ahmed Al‑Tayeb, kwa lengo la kuziunga mkono taasisi za kuhifadhi Qur’ani, kuimarisha nafasi yake katika kuhudumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kujiandaa kwa shughuli za Qur’ani za msimu wa kiangazi ambazo zimepokelewa kwa mwitikio mkubwa katika Maktab na halaqa za kuhifadhi Qur’ani katika majimbo mbalimbali ya nchi.
Mradi huu unaongozwa na Ahmed Al‑Sharkawi, mkuu wa Idara ya Taasisi za Al‑Azhar, chini ya usimamizi wa Sheikh Ayman Abdel Ghani, Naibu Mufti Mkuu wa Al‑Azhar. Utekelezaji wake ulianza tarehe 20 Juni katika jimbo la Luxor nchini Misri.
Kwa mujibu wa mpango huo, shughuli za ugawaji zimefanyika Jumpili na Jumatatu katika jimbo la Qena, na pia katika majimbo ya Sohag, Assiut na Minya, kabla ya kuendelea katika majimbo mengine kote Misri.
Mradi huu maalumu unasimamiwa na Al‑Azhar katika maeneo yote ya Misri na unalenga kuwapatia wanaojifunza Qur’ani pamoja na halaqa za hifdhi nakala zinazohitajika za Misahafu.
Abu Yazid Salameh, mmoja wa maafisa watendaji wa mradi huo, amesema kuwa mchakato wa ugawaji unafanywa kwa kuzingatia tathmini ya mahitaji halisi ya kila jimbo, jambo linalosaidia kukidhi ipasavyo mahitaji ya vituo vya kuhifadhi Qur’ani.
Kwa upande wake, Sheikh Ayman Abdel Ghani ameeleza kuwa mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Al‑Azhar wa kuitunza Qur’ani Tukufu na kuwasaidia wahudumu wa Qur’ani, huku ukichangia kujenga jamii yenye uelewa mpana zaidi wa dini na yenye uthabiti wa maadili.
Naye Ahmed Al‑Sharkawi amesisitiza kuwa idara hiyo inatoa kipaumbele maalumu kwa shughuli za Qur’ani za msimu wa kiangazi, kwa kuwa ni fursa muhimu kwa vijana kutumia vyema wakati wao wa mapumziko katika kuhifadhi Qur’ani, kujifunza kanuni na adabu za usomaji wake, na kujenga maadili mema pamoja na tunu za kijamii na kitaifa zinazotokana na mafundisho ya Wahyi.
/3497925