Wananchi wa eneo la Qatif walisisitiza kuendeleza kumbukumbu za Ashura tangu usiku wa kwanza wa mwezi wa Muharram kwa kuandaa angalau majlisi 600 za kumbukumbu ya Imam Hussein (AS).
Kwa mujibu wa tovuti ya Naba, mikusanyiko hiyo inaashiria kujitolea kwa jamii ya Mashia wa eneo hilo katika kulinda ibada zao za kidini na utambulisho wao wa Kiislamu.
Kulingana na uchunguzi wa uwanjani pamoja na takwimu zilizochapishwa na jukwaa la “Masurat”, majlisi hizo zilifanyika katika misikiti, Husseiniyya (kumbi za hafla za kidini katika jamii za Mashia) pamoja na nyumba za watu katika miji, vijiji na mitaa mbalimbali ya Qatif.
Hali hii inaonyesha msimamo na azma ya wakazi wa eneo hilo ya kuendelea kuadhimisha majlisi za maombolezo ya Muharram. Wahubiri katika majlisi za usiku wa kwanza wa Muharram walisisitiza umuhimu wa kuendeleza kumbukumbu na ujumbe wa Ashura bila kujali gharama au changamoto zinazoweza kujitokeza, pamoja na haja ya kuyatekeleza mafundisho ya harakati ya Imam Hussein (AS) katika maisha ya kijamii.
Ripoti zilizochapishwa kuhusu suala hilo zinaonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi kwa majlisi hizo za maombolezo, ambapo hata mikusanyiko midogo ilihudhuriwa na idadi kubwa ya waombolezaji.
Mashia wa Qatif wanashiriki katika ibada za Muharram huku, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, vyombo vya usalama vya Saudi Arabia vikiweka vikwazo fulani juu ya uendeshaji wa ibada hizo. Hatua hizo zinadaiwa kujumuisha kuwekwa kwa vituo vya ukaguzi barabarani, kudhibiti harakati za baadhi ya raia, kuzuia baadhi ya programu za pamoja, kuondoa alama na bendera za maombolezo katika barabara za umma, na pia kuzuia kuanzishwa kwa baadhi ya vituo vya kuwakaribisha washiriki wa majlisi.
Licha ya changamoto na vizuizi hivyo, waandaaji wa majlisi pamoja na wanaharakati wa kidini wamejitahidi kuendeleza ibada za Muharram kwa kutumia njia mbadala. Njia hizo ni pamoja na kufanya majlisi katika maeneo binafsi, kuweka bendera katika njia za ndani, na kutumia majukwaa ya mtandaoni. Katika muktadha huo, zaidi ya majlisi 100 za maombolezo zimerushwa moja kwa moja kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya majlisi za maombolezo za Imam Hussein (AS) katika Qatif imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Eneo la Qatif pamoja na maeneo ya mashariki ya Saudi Arabia yanachukuliwa kuwa vituo vikuu vya uwepo wa jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo. Kila mwaka katika mwezi wa Muharram, maeneo hayo huwa mwenyeji wa majlisi nyingi za maombolezo pamoja na programu za kitamaduni na kidini zinazohusiana na ujumbe na harakati ya Ashura.
/3497887