IQNA

Usajili wa Mazuwar Wairani kwa ajili ya Matembezi ya Arbaeen kuanza 30 Juni

19:09 - June 22, 2026
Habari ID: 3482389
arbaeen
IQNA – Makao Makuu ya Arbaeen ya Imam Hussein (AS) nchini Irani yametangaza rasmi tarehe za kuanza kwa usajili wa waumini wanaokusudia kushiriki katika matembezi ya Arbaeen ya mwaka huu nchini Iraq.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi, Makao Makuu hayo yamesisitiza kuwa, kwa kufuata mwongozo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, wamejipanga kikamilifu ili kuhakikisha safari ya mazuwar wa Arbaeen ya mwaka huu inakuwa ya “nyepesi, salama, nafuu, na yenye heshima.”

Taarifa hiyo imebainisha kuwa usajili wa kushiriki katika hija hii ya Arbaeen kupitia mfumo wa “Samah” utaanza saa 3:00 asubuhi ya siku ya Jumanne, Juni 30, 2026, sawa na tarehe 15 Muharram 1448 Hijria.

Viongozi wamesisitiza kwa msisitizo mkubwa kuwa ni lazima kwa kila mwenye lengo la kushiriki Arbaeen kujiandikisha katika mfumo wa Samah ili kuweza kufaidika na huduma zote muhimu zitakazotolewa njiani.

Aidha, shughuli za kuwasafirisha mahujaji kuelekea nchini Iraq zitaanza tarehe 25 Julai na kuhitimishwa tarehe 6 Agosti.

Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia katika siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, kukumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia.

Arbaeen ni moja ya ziara kubwa zaidi za kidini duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na idadi kubwa ya Masunni na pia wafuasi wa dini nyingine, hufanya safari ya miguu kuelekea Karbala wakitokea miji mbalimbali nchini Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itaangukia tarehe 4 Agosti.

Ikumbukwe kuwa katika mwaka wa 2025, mahujaji wapatao milioni 4 kutoka Irani walishiriki katika tukio hili tukufu la matembezi ya Arbaeen.

3497913

Habari zinazohusiana
captcha