Kufuatia uamuzi wa jaji wa mahakama ya shirikisho uliotolewa Alhamisi kumwachia huru Salah Sarsour kutoka kizuizi cha ICE, kiongozi huyo wa msikiti mkubwa zaidi huko Wisconsin amerejea nyumbani.
Sarsour alirejea Milwaukee akitokea Indiana Alhamisi jioni. Siku ya Ijumaa, alihudhuria swala na kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kuachiliwa kwake.
Baada ya siku 80 akiwa mikononi mwa mamlaka za uhamiaji, Sarsour alieleza kuwa kurejea katika msikiti wake wa nyumbani na kuswali pamoja na ndugu na jamaa zake ni jambo alilokuwa akiliombea kwa muda mrefu.
“Alhamdulillah, hatimaye nimerudi, na niko hapa pamoja na wajukuu zangu na familia yangu,” alisema Sarsour kwa hisia.
Sarsour amekuwa rais wa Jumuiya ya Kiislamu ya Milwaukee kwa miaka mitano iliyopita. Yeye ni mwenyeji wa Ukingo wa Magharibi (West Bank) katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel, lakini amekuwa akiishi Marekani kama mkazi halali wa kudumu kwa zaidi ya miaka 30.
Sarsour anaamini kuwa utetezi wake wa haki za Wapalestina ndiyo sababu kuu ya yeye kulengwa, hatua ambayo inakiuka haki ya uhuru wa kusema.
Alikamatwa na ICE mwezi Machi, huku serikali ikidai kuwa yeye ni tishio kwa sera za kigeni. Madai hayo yanarejea nyuma hadi miaka ya 1989 na 1995, ambapo mahakama ya kijeshi ya utawala wa Israel ilimtia hatiani kwa madai ya makosa dhidi ya vikosi vya Israel.
“Hizi ni tuhuma za kizamani za miaka 30 zilizopita ambazo wamezifukua sasa hivi,” alisema wakili wake, Luna Droubi. “Wanajua fika kuwa ni za uongo. Kwa kweli, walichagua kutoziamini tuhuma hizo mara kadhaa katika kipindi chote cha miaka 30 ambacho Bw. Sarsour amekuwa nchini hapa.”
Sarsour anakanusha kutenda makosa hayo na kusema kuwa hayajawahi kuathiri sifa zake za kupata uraia kwa zaidi ya miaka 25. Alionyesha kuridhishwa na uamuzi wa jaji wa kumwachia huru.
“Namna alivyochagua kuwa jaji mwadilifu, kwa kweli, amenipa matumaini katika mfumo huu,” Sarsour alisema. “Tunamshukuru Mungu kwamba bado tuna watu wema wanaoweza kutoa hukumu ya haki kwa ajili ya mustakabali mwema.”
Kuachiliwa kwa Sarsour hakumaanishi kuwa suala la kufukuzwa kwake nchini (deportation) limetatuliwa. Wakili wake alisema wanapanga kuendelea na hatua za kisheria ili kuhakikisha Sarsour anabaki Marekani, na wataendelea kushughulikia kesi yake ya uhamiaji na kesi ya shirikisho.
“Tunaamini kwa dhati kuwa jaji atatoa uamuzi wa mwisho kwamba haki za kikatiba za Salah Sarsour zilivunjwa,” Droubi alisema.
Sarsour alikiri kuwa bado kuna safari ndefu mbele, lakini anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa ya kurejea nyumbani akiwa na familia yake.
3497901