Akizungumza na IQNA, Adnan Abdullah Al-Junaid, mwandishi na mtafiti wa kisiasa wa Yemen, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi Waarabu na Huru, na mjumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Wataalamu na Wachambuzi wa Kisiasa, alisema kuwa mhimili huu unavuka mipaka ya madhehebu na tofauti za kidini.
Amesisitiza kuwa umoja ndio sharti la msingi kwa ajili ya usalama na uhai wa Umma wa Kiislamu katika zama hizi za tabia za uadui kutoka kwa “ubeberu au uistikbari wa kimataifa”.
Amesema kuwa Ayatullah Khamenei alizingatia kwa dhati suala la umoja wa Umma wa Kiislamu na ukaribu kati ya madhehebu ya Kiislamu, na kwa muktadha huo, alikuwa mmoja wa wafadhili wakuu wa kuandaliwa kwa Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu nchini Iran.
“Aidha, Jukwaa la Kimataifa la Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu lilianzishwa mwaka 1990 kwa ubunifu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi. Kwa miaka mingi, jukwaa hili limekuwa na nafasi muhimu katika kupunguza mivutano na tofauti za kidini, kuunga mkono kadhia ya Palestina na Al-Quds, na kuendeleza umoja wa Umma wa Kiislamu.”
Al-Junaid alibainisha kuwa Kiongozi Shahidi aliamini kuwa umoja si suala la kimaadili wala kaulimbiu ya kisiasa tu, bali ni sharti la kuunusuru Umma wa Kiislamu dhidi ya mashambulizi ya kimataifa.
“Aliuchukulia umoja kama ngao dhidi ya miradi ya kuibua mifarakano baina ya Waislamu na pia ni na silaha ya kimkakati katika kukabiliana na utawala wa kidhalimu wa Israel, na aliamini kuwa adui hashindi kwa nguvu zake pekee, bali hujaribu kutawanya na kudhoofisha jamii ya Kiislamu kupitia mgawanyiko wa ndani. Umma ulioungana pekee ndio unaoweza kulinda imani yake, mamlaka yake, na uamsho wake. Kwa hivyo, aliona umoja kama wajibu wa kidini na hitaji la kihistoria ambalo haliwezi kuahirishwa.”
Alipoulizwa ni nini Kiongozi Shahidi aliona kama vikwazo vikuu vya umoja baina ya madhehebu za Kiislamu, alisema Ayatullah Khamenei alibainisha vikwazo hivyo kwa usahihi wa mwanamapinduzi mwenye uelewa. “Kwa mtazamo wake, vikwazo hivi ni pamoja na: ushabiki wa kimadhehebu, ujinga, na kugeuza tofauti kuwa masuala ya kisiasa.”
“Shahidi Khamenei aliamini kuwa madola ya kibeberu huibua hitilafu, kisha huzifadhili na kuzichochea kupitia majukwaa ya mamluki na vyombo vya habari vyenye sumu. Alionya dhidi ya kugeuza tofauti za kiitikadi kuwa mipasuko katika jamii ya Waislamu na akasisitiza kuwa adui hatari zaidi ni ujinga pale unapojificha katika vazi la dini. Kwa mtazamo wake, mapambano huanza katika uwanja wa uelewa kabla ya kuhamia katika uwanja wa vita.”
Mchambuzi huyo wa Yemen aliendelea, “Mapambano dhidi ya mgawanyiko na kutokuwa na umoja yalikuwa mada endelevu katika hotuba za Shahidi Ayatullah Khamenei, si msimamo wa muda. Aliona ushabiki wa kimadhehebu, bila kujali mwonekano wake, kama usaliti kwa Umma, na kila neno linalochochea faraka, kama risasi iliyolenga moyo wa mapambano. Kwa mtazamo wake, mgawanyiko ni hatari zaidi kuliko uvamizi wa kijeshi kwa sababu huharibu jamii kutokea ndani.”
Al-Junaid amesema Kiongozi Shahidi aliunganisha umoja na heshima kupitia uhusiano wa kihistoria; taifa lililoungana huweka masharti yake, wakati taifa lililotawanyika huwa chini ya amri za wengine.
“Aliamini kuwa maendeleo ya kisayansi, kijeshi, na kisiasa hayawezi kutokea katika mazingira yaliyotawanyika. Umoja hubadili mataifa kuwa nguvu inayojishughulisha, na mgawanyiko huyafanya kuwa uwanja wa ushawishi na migogoro ya uwakilishi (proxy conflicts).”
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuleta madhehebu ya Kiislamu karibu zaidi, alisema, “Hakutegemea kaulimbiu pekee, bali alichukua hatua kuelekea vitendo vya kitaasisi na vilivyopangwa. Aliunga mkono makongamano ya umoja na mazungumzo ya kidini na kutoa fatwa kali zinazokataza matusi dhidi ya matukufu na nembo za kidini. Alifungua milango ya kubadilishana maarifa ya kisayansi na kidini. Hivyo, alibadilisha umoja kutoka dhana ya kinadharia na kuufanya kuwa mazoezi ya kila siku.”
Aliendelea kusema kuwa kwa mtazamo wa Kiongozi Shahidi, nafasi ya wanazuoni na wasomi wa kidini katika kufanikisha ukaribu kati ya madhehebu ilikuwa muhimu sana.
“Aliweka dhima ya kihistoria kwenye mabega ya wanazuoni kuwa walinzi wa elimu na si wafanyabiashara wa tofauti. Aliwaita wanazuoni kutatua tofauti kwa mantiki, si kuzichochea. Aliwaita pia wanazuoni kuongoza Umma kuelekea kwenye misingi ya pamoja, si kuelekea kwenye migogoro. Aliona mimbari kama amana, kauli kama dhima, na kunyamaza kimya mbele ya tofauti kama kushiriki katika kuhudumia maslahi ya ubeberu waa kimataifa.”
3498061