Tukio hilo liliandaliwa kwa lengo la kuonyesha uwezo wa wanawake Waislamu katika nyanja za kiuchumi, kitamaduni na kijamii.
Moja ya sehemu muhimu za hafla hiyo ilikuwa maonyesho yaliyoshirikisha vibanda vingi vilivyoendeshwa na wanawake Waislamu. Katika vibanda hivyo, bidhaa mbalimbali zilioneshwa, zikiwemo vyakula vya jadi, pipi na vitafunwa vya kienyeji, mimea ya tiba asilia, mazao ya kilimo, kazi za mikono, bidhaa za nyumbani pamoja na bidhaa za afya na urembo.
Maonyesho hayo yalionyesha jinsi wanawake Waislamu wa Thailand walivyoweza kubadilisha ujuzi wao wa jadi na wa nyumbani kuwa biashara ndogo ndogo za kifamilia. Shughuli hizi si tu zinachangia kuimarisha uchumi wa familia, bali pia zinatoa fursa nzuri ya kutambulisha na kuuza bidhaa za kienyeji.
Tukio hilo halikujikita katika masuala ya kiuchumi pekee, bali pia lilikuwa fursa ya kuonesha urithi wa kitamaduni wa Waislamu wa Thailand. Kupitia uwasilishaji wa bidhaa za jadi na kazi za mikono, washiriki waliwasilisha sehemu ya utamaduni na utambulisho wa jamii za Kiislamu za maeneo yao.
Vibanda mbalimbali pia vilitambulisha mila na desturi za maeneo na misikiti iliyoshiriki, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kuurithisha kwa vizazi vijavyo.
Sifa nyingine ya tukio hilo ilikuwa uwepo wa wawakilishi kutoka misikiti na jamii mbalimbali za Kiislamu kutoka maeneo tofauti ya nchi, hali iliyolifanya tukio hilo kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu, kupanua ushirikiano na kuimarisha mahusiano ya kijamii miongoni mwa wanawake Waislamu.
Kwa upande mwingine, mbali na programu za kiutamaduni na kiuchumi, sehemu ya hafla hiyo ilitengwa kwa ajili ya huduma za afya na utoaji wa elimu ya afya. Vikundi kutoka vituo maalumu pamoja na wanafunzi wa sayansi za afya walitoa huduma mbalimbali kwa washiriki kupitia ushauri wa afya na uchunguzi wa awali wa kitabibu.
Thailand ni miongoni mwa nchi muhimu za Asia ya Kusini Mashariki yenye mamilioni ya Waislamu. Sehemu kubwa ya Waislamu wa Thailand wanaishi katika maeneo ya kusini ya nchi hiyo pamoja na jijini Bangkok, ambapo taasisi za Kiislamu na misikiti zina nafasi muhimu katika kuratibu shughuli za kidini, kielimu, kitamaduni na kijamii. Makadirio yanaonyesha kuwa idadi ya Waislamu nchini Thailand ni kati ya milioni 4 hadi 5, sawa na takribani asilimia 6 hadi 7 ya jumla ya watu wa nchi hiyo.
/3497889