Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Malaysia, Mohamad Sabu, alimsifu Kiongozi huyo Shahidi, akimwelezea kama kiongozi ambaye ushawishi wake ulienea mbali zaidi ya mali za kimwili, na ambaye urithi wake utaendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Katika mahojiano yaliyofanyika wakati wa msafara wa mazishi ya Shahidi Khamenei, Sabu alimwelezea marehemu Kiongozi huyo kama “mtu tajiri zaidi duniani,” akifafanua kuwa utajiri wake wa kweli haukuwa katika miliki za kidunia, bali katika mapenzi ya dhati na uungaji mkono wa watu wa Iran.
“Hakuhitaji gari wala nyumba,” alisema Sabu. “Iran nzima na watu wake milioni 90 walikuwa pamoja naye. Utajiri wake ulikuwa ni Uislamu na kujitolea kwake katika kuhudumia Uislamu.”
Waziri huyo wa Malaysia alionyesha imani kuwa itikadi alizozipigania Shahidi Khamenei zitaendelea kudumu, akisema kuwa Uislamu utaendelea kusonga mbele kupitia nuru ya mwongozo wake. Alimwelezea marehemu kiongozi huyo kama “kiongozi wa kweli” aliyefuata nyayo za Mtume Muhammad (SAW), akiongeza kuwa alimwona Shahidi Khamenei kama “kinara wa uamsho wa Kiislamu katika Ummah wa Kiislamu wa leo.”
Akizungumzia masuala ya kimataifa, Sabu aliikosoa vikali Marekani na undumilakuwili wake kuhusu haki za binadamu. Alisema kuwa nchi zinazodai kutetea haki za binadamu zimekaa kimya kuhusu mauaji ya raia, wakiwemo watoto. Waziri huyo wa Malaysia pia alisisitiza kuwa mienendo ya nguvu za kimataifa inabadilika, akidai kuwa ushawishi wa Marekani unadidimia na kwamba hata nchi nyingi za Ulaya haziko tena katika mstari mmoja na Washington.
Akirejelea mzozo unaohusisha Iran, Israel, na Marekani, Sabu alisema anaamini kuwa mzozo huo ni mwanzo wa mabadiliko mapana zaidi katika uwiano wa nguvu duniani. Alihitimisha kwa kutoa matumaini kuwa Iran itachukua nafasi ya uongozi katika kuunda mustakabali wa eneo hilo na ulimwengu kwa upana.
3498094