Allamah Muhammad Hussein Fadhlullah, kiongozi mkuu wa kidini nchini Lebanon amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Pakistan ambayo yamesababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia yoyote.
Mwandishi wa IQNA nchini Lebanon ameripoti kuwa mwanazuni huyo mashuhuri wa kidini amesisitiza kuwa magaidi hao wanafuata fatuwa za mashekhe wenye mitazamo finyu ya chuki za kimadhehebu ambao hawaelewi vyema kitabu cha Mwenyezi Mungu na suna za Mtume Muhammad (saw).
Allamah Fadhlullah amewataka wanazuoni wa Kiislamu kulaani jinai hiyo na kuchukua hatua za kuwazindua Waislamu na kuwaongoza katika umoja na mshikamano wa Kiislamu ambayo ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ubeberu wa kimataifa.
Amesema kuwa Waislamu wa Kishia wa Pakistan wamekuwa wakikabiliwa na mauaji ya mara kwa mara kutokana na fatuwa zinazohalalisha damu yao zinazotolewa na mashekhe wanaowakufurisha Waislamu.
Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameitaka pia serikali ya Pakistan kusimamisha mauaji hayo yanayokiuka misingi ya Uislamu.
Ni vyema kukumbusha kuwa siku kadhaa zilizopita msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mkoa wa Punjab ulishambuliwa kwa bomu ambalo lilisababisha vifo vya Waislamu kadhaa na kujeruhi makumi ya wengine. 385026