IQNA

Maulamaa wa Kishia wa Saudia wailaumu serikali kwa ubaguzi wa kimadhehebu na kiuchumi

17:28 - April 23, 2009
Habari ID: 1768846
Sheikh Hassan Saffar na Taufiq al A'miri, ambao ni miongoni mwa maualamaa wakubwa wa Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia wameikosoa serikali ya Riyadh kwa kubana shughuli za kidini na kisiasa za Mashia nchini humo na wametoa wito wa kuboreshwa hali ya kiuchumi ya wafuasi wa madhehebu hiyo ya Kiislamu.
Sheikh Taufiq al A'miri ameashiria udharura wa kutupiliwa mbali ubaguzi wa kimadhehebu katika masuala ya uendeshaji wa nchi na akataka kutambuliwa rasmi madhehebu ya Shia kama yalivyo madhehebu nne za Kisuni nchini Saudi Arabia.
Sheikh al A'miri ametilia mkazo udharura wa kuwepo uhuru wa kidini na kimadhehebu nchini Saudia kwa mujibu wa sheria za kimataifa na akasema: Mashia wa Saudi Arabia wanataka kuwa na nafasi katika bunge na mabaraza ya miji na vijiji kama walivyo ndugu zao wa Kisuni.
Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu ambaye amekwisha kamatwa na kufungwa jela mara mbili nchini Saudia kwa sababu ya kuikosoa waziwazi serikali, amesema kuwa operesheni za kuwatia nguvuni mara kwa mara Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo kwa visingizio mbalimbali zinakiuka makubaliano ya haki za binadamu na sheria za Kiislamu.
Kwa upande mwingine Sheikh Hassan Saffar ambaye ni Imam wa Ijumaa wa mji wa Qatif mashariki mwa Saudia ameitaka serikali kutoa suhula za kiuchumi kwa Waislamu wa Kishia na kuwapa mikopo ya muda mrefu kwa shabaha ya kukidhi mahitaji yao ya kimaisha kama maji na nishati.
Ripoti iliyotolewa mwaka 1996 na shirika moja la kimataifa la kutetea haki za binadamu ilisema kuwa serikali ya Saudi Arabaia ni serikali ya kidhalimu na kikatili ambayo sifa yake kuu ni "kuwachukia wafuasi wa madhehebu ya Shia". 393095
captcha