IQNA

Kikao cha kimataifa cha 'Qur'ani na Nafasi yake katika Kurekebisha Jamii' chafanyika Yemen

8:01 - May 05, 2009
Habari ID: 1773992
Kikao cha kimataifa cha kuchunguza nafasi ya Qur'ani katika kurekebisha jamii kilianza siku ya Jumapili katika Taasisi ya Taaluma na Utamaduni ya as-Said ya mjini Taiz nchini Yemen.
Kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo, Ahmad Abdul Karim al-Kubeisi, mhadhiri wa Taaluma ya Qur'ani katika Chuo cha Fasihi cha Ibb ametoa hotuba katika kikao hicho na kusema kuwa usawa, uadilifu na uhuru ni miongoni mwa nguzo muhimu za dini ya Kiislamu, nguzo zenye thamani kubwa ambazo zinaweza kutumika kwa lengo la kurekebisha jamii. Amesema kuwa kurekebisha jamii ni ujumbe muhimu zaidi wa Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha historia, jambo ambalo amesema limeilinda jamii na kuiweka mbali na mambo ya upotofu wa kifikra na kimaadili. Amesema urekebishwaji wa fikra katika jamii ni jambo lililo na umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa iwapo fikra potofu zitaruhusiwa kuenea katika jamii, zitachochea mielekeo ya utumiaji mabavu katika jamii hiyo. Ameelezea masikitiko yake makubwa kwamba kwa bahati mbaya hiyo ndiyo hali inayotawala katika nchi nyingi za Kiislamu na hivyo kuzusha hitilafu na mifarakano miongoni mwao.
Mtafiti huyo wa masuala ya Qur'ani wa Yemen amesisitiza kwamba, urekebishaji wa jamii unahitajia masuala mbalimbali, ambapo malezi ya wahubiri wenye ufahamu wa fikra na masuala ya Kiislamu ni miongoni mwa masuala hayo. Amesema, umuhimu huu unatokana na udharura wa wahubiri wa Kiislamu kutambua thamani halisi za Kiislamu ma kuakisiwa kwa thamani hizo katika vitendo na mienendo yao maishani.
Ahmad Abdul Karim al-Kubeisi amesema jambo hilo lina athari kubwa katika kuwavutia watu wanaofanyiwa uhubiri, ili kuwafanya waweze kufuata fikra na njia sahihi za maisha.
Kikao hicho kimefanyika katika fremu ya tamasha la 11 la kimataifa la kiutamaduni na Kiislamu la as-Said, kikao ambacho kimehudhuriwa na wataalamu na watafiti wa Qur'ani kutoka nchi za Yemen, Saudi Arabia, Imarati na Kuwait. 399321
captcha