IQNA

Udharura wa ulimwengu wa Kiislamu kufanya juhudi za kunyanyua nafasi yake katika ngazi za kimataifa

9:45 - May 06, 2009
Habari ID: 1774575
Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC amesisitiza katika kikao cha utangulizi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, juu ya udharura wa ulimwengu wa Kiislamu kufanya juhudi za kunyanyua nafasi yake katika upeo wa kimataifa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la jumuiya hiyo, Ihsanoglu amesema kuwa katika siku zilizopita Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imekuwa ikijishughulisha tu na uandaaji wa vikao na utoaji wa mapendekezo lakini hii leo jumuiya hiyo imebadili sera hiyo na kujishughulisha zaidi na suala la kushirikiana kwa kiwango kikubwa na serikali na vilevile mashirika ya kimataifa na kiraia. Katibu Mkuu huyo pia ameashiria matatizo na changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na kutahadharisha kwamba iwapo utawala haramu wa Israel utaendeleza hujuma yake dhidi ya Baitul Muqaddas, Waislamu watapoteza Quds Tukufu, kwa sababu kuna mpango kabambe na madhubuti unaopangwa kutekelezwa na Wazayuni katika eneo hilo, nyuma ya pazia la uchokozi na uharibifu unaotekelezwa na utawala wa Israel katika eneo hilo takatifu.
Ihsanoglu ameashiria juhudi za jumuiya ya OIC za kupambana na uchochezi wa chuki dhidi ya Uislamu na kuongeza kuwa hii leo watu wengi duniani wamefahamu vyema kwamba kueneza chuki hizo kunahatarisha uthabiti na usalama wa dunia.
Kikao hicho kimejadili ajenda ya kikao kijacho cha 36 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC ambacho kimepangwa kufanywa tarehe 23 hadi 25 za mwezi huu wa Mei mjini Damascus, Syria. 399992
captcha