IQNA

OIC yataka kusimamishwa operesheni za kufanywa mji wa Quds kuwa wa Kiyahudi

13:50 - May 12, 2009
Habari ID: 1777410
Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC siku ya Alkhamisi aliitumia ujumbe kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani akiitaka serikali ya Washington kuushinikiza utawala haramu wa Israel usimamishe mara moja mipango yake ya kuharibu utambulisho halisi wa Kiarabu na Kiislamu wa mji mtakatifu wa Quds na kuufanya kuwa wa Kiyahudi.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Saudi Arabia SPA Ihsanoglu amesema katika ujumbe huo kwamba, operesheni haribifu za utawala wa Israel za kubomoa nyumba za Wapalestina wanaoishi Quds na ujenzi wa vitongoji vya Mayahudi katika ardhi za Wapalestina, zinakiuka wazi sheria za kimataifa na Azimio la Geneva na hivyo kufanya juhudi za kubuniwa kwa taifa huru la Palestina kuwa jambo lisilowezekana. Amesema katika ujumbe huo kwamba, hatua hizo za utawala wa Israel zinahatarisha usalama na uthabiti wa wa Mashariki ya Kati na kuvuruga kabisa juhudi za kimataifa ambazo zimefanyika kwa madhumuni ya kuleta amani katika eneo. Katibu Mkuu huyo ameashiria makala iliyoandikwa hivi karibuni katika gazeti la Israel la Haaretz kwamba operesheni za ujenzi zinazotekelezwa na utawala wa Israel katika eneo la Quds zina lengo la kubadili kabisa sura ya Kiislamu na Kiarabu katika mji huo mtakatifu, na kusema kuwa, katika mipango inayotekelezwa kisiri katika mji huo, utawala ghasibu wa Israel una lengo la kujenga vitongoji vipya katika mji huo na kuzipa barabara na viwanja yake vya starehe majina mapya ya Kiyahudi, na hivyo kufuta yale ya Kiarabu na Kiislamu. Gazeti hilo limesema, jambo hilo hatimaye litawalazimu Wapalestina kukubali rasmi kuwa mji huo ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Ihsanoglu amesisitiza mwishoni mwa ujumbe wake kwamba mipango ya kiuadui ya utawala wa Israel inatekelezwa katika hali ambayo kwa upande mmoja, Marekani inazungumzia suala la kuimarisha uhusiano wake na ulimwengu wa Kiislamu, na kwa upande wa pili imenyamazia kimya hatua hizo haribifu na haramu za utawala wa Kizayuni dhidi ya matukufu ya Kiislamu huko Palestina. 403234
captcha