Abdul Amir al-Shammari, ambaye pia ni Mkuu wa Kamati Kuu ya Usalama kwa Maadhimisho haya ya watu mamilioni, alitoa agizo la kuendeleza maandalizi ya mwisho ili kuhakikisha amani na utulivu wakati wa tukio la Arbaeen.
Aliongoza kikao kikubwa kilichofanyika kwa njia ya mtandao, ambacho kilihudhuriwa na manaibu wa wizara, washauri, makamanda wa usalama, pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali.
Katika kikao hicho, waziri alisisitiza kukamilisha maandalizi ya mwisho ya kiusalama kwa ajili ya hafla ya Arbaeen, na kutangaza utekelezaji wa mipango maalum ya kiutawala na uratibu kwa ajili ya tukio hili takatifu.
Pia alisisitiza umuhimu wa kupata suluhisho sahihi kwa changamoto kama vile ajali za barabarani na matukio ya moto, huku akitambua juhudi kubwa za Idara ya Usafiri na Usalama Barabarani katika kuhakikisha mzunguko mzuri wa mahujaji.
Kwa kusisitiza kwamba mafanikio halisi ya tukio hili yapo katika kupunguza taabu wanazopata za wafanyaziyara na kulinda maisha ya waombolezaji, Al-Shammari alieleza kuwa huu ni ujumbe wa kiroho unaopaswa kutekelezwa kwa njia bora kabisa, kuanzia mipakani hadi katika mji mtukufu wa Karbala.
Aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imetuma uwezo wake wote kwa ajili ya kuwatumikia na kuwalinda mahujaji, ikijumuisha usimikaji wa kamera za uangalizi, kuimarisha vikosi vya usalama kwa rasilimali watu, magari, na vifaa mbalimbali.
Al-Shammari pia aliamuru manaibu wake wote, makamanda na viongozi wa usalama kuwa mashinani, kushiriki moja kwa moja na kukagua hali ya usalama katika maeneo yote.
Akasema kuwa mafanikio ya mpango huu wa kiusalama ni muhimu sana, hasa ikizingatiwa uwepo wa mamilioni ya wafanyaziyara kutoka ndani na nje ya Iraq, na akasisitiza kuwa hilo linawezekana tu kupitia usambazaji sahihi wa vikosi na usimamizi wa hali ya juu.
Aidha, alieleza umuhimu wa kuwepo kwa kikamilifu kwa vikosi vya upelelezi katika mstari wa mbele wa usalama kwenye maeneo yote ya msafara, na kwamba vikosi hivyo vinapaswa kutenda kwa mujibu wa uzito wa tukio hili kubwa la mamilioni ya watu.
Katika taarifa nyingine inayohusiana, Kamandi ya Polisi ya Karbala imetangaza kuwa zaidi ya Mawkib 14,000 kutoka Iraq na Mwakib 205 kutoka mataifa ya kigeni wamesajiliwa ili kutoa huduma kwa mahujaji wa Arbaeen mwaka huu.
Mawkib ni vituo vya huduma vilivyo katika maeneo ya kidini ya Waislamu wa madhehebu ya Shia au wakati wa matukio ya kidini ya Mashia ambapo wafanyaziara na watu wanaweza kupokea chakula, chai, na sharbat (vinywaji vitamu) na kupata sehemu ya kupumzika.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia siku ya arobaini baada ya siku ya Ashura, kuenzi ushahidi wa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu wa Kishia.
Ni mojawapo ya hija kubwa zaidi duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na baadhi ya Masunni na hata watu wa dini nyingine, huelekea kwa miguu hadi Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itasadifiana na tarehe 14 Agosti.
3494131