Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Wamarekani (CAIR), ambalo ndilo shirika kubwa zaidi la kutetea haki za kiraia za Waislamu nchini Marekani, siku ya Jumapili lililaani pia mauaji ya kinyama dhidi ya raia waliokuwa wakitafuta msaada wa chakula kwa ajili ya familia zao, pamoja na uvamizi wa makusudi wa Msikiti Mtakatifu wa Al-Aqsa unaofanywa na makundi ya Wazayuni na Wayahudi wenye misimamo mikali.
Taarifa zinaeleza kuwa Wapalestina wengine sita wamefariki dunia kutokana na njaa kali inayotumika kama silaha dhidi ya raia wa Gaza, na kufanya idadi ya waliokufa kwa njaa kufikia watu 175, wakiwemo watoto 93. Mashambulizi ya Israel katika Gaza jana pekee yamesababisha vifo vya angalau watu 92, wakiwemo wengi waliokuwa wakitafuta misaada ya kibinadamu.
Katika tamko lake rasmi, CAIR ilisema:
“Ulimwengu hauwezi kuendelea kufumba macho mbele ya mauaji yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza. Utawala wa Kizayuni kutumia njaa kama silaha ya vita tayari umesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 175 ambapo karibu nusu ni watoto. Mauaji ya leo ya watu waliokuwa wakitafuta msaada wa chakula ni ushahidi mwingine wa kikatili kuwa mzingiro wa Israel siyo tu kinyume na sheria za kimataifa, bali ni fedheha kwa utu wa binadamu.”
“Tunalaani kwa kauli kali kabisa uvamizi wa makusudi wa Msikiti wa Al-Aqsa unaofanywa na wavamizi wa Kizayuni, ambao ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya haki ya Waislamu duniani kote ya kuabudu kwa amani.”
“Tunatoa wito kwa utawala wa Rais Trump pamoja na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti: kuondoa mzingiro wa Gaza, kuhakikisha msaada wa kibinadamu unafika kwa walio hatarini, na kuiwajibisha Israel kwa uhalifu wa kivita dhidi ya raia. Kauli zisizo na matokeo hazitoshi tena — lazima kuwe na hatua na adhabu.”
Wiki iliyopita, CAIR ilipongeza hatua ya Slovenia kupiga marufuku biashara yote ya silaha na Israel, ikisema kuwa huo ni uthibitisho kwamba barani Ulaya “kumekucha polepole kuhusu mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza.”
CAIR pia ilikaribisha tangazo la Serikali ya Canada kwamba inapanga kulitambua rasmi taifa la Palestina, na ikalaani kauli ya Rais Trump ya kutishia kufuta makubaliano ya kibiashara na Canada kutokana na uamuzi huo jambo walilosema linaonesha wazi kuwa “utawala wake unaipa Israel kipaumbele kuliko hata maslahi ya taifa la Marekani.”
Mwezi uliopita, CAIR ilikaribisha pia mpango wa serikali ya Ufaransa wa kulitambua taifa la Palestina kama nchi huru.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza katika takwimu zake mpya kwamba: Wapalestina 60,839 wameuawa shahidi na 149,588 kujeruhiwa tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7,2023.