Katika taarifa aliyotoa Ijumaa jioni, Ayatullah Sistani alisema: “Baada ya karibu miaka miwili ya mauaji na uharibifu usiokoma, ambao umesababisha vifo na majeruhi kwa mamia ya maelfu ya watu, na kubomoa miji na makazi bila idadi, Wapalestina walioko Gaza wanaishi katika mazingira ya kutisha.”
Ameonya kuwa baa la njaa katika eneo hilo lililozingirwa la pwani limeenea kwa kiwango cha kutisha kiasi kwamba hakuna sehemu yoyote ya jamii iliyobaki bila kuathirika.
Ayatullah Sistani amesisitiza kuwa, "Hakuna linalotarajiwa kutoka kwa majeshi ya uvamizi ya Israel isipokuwa ukatili wa kinyama katika juhudi zao za kuwang’oa kwa nguvu wananchi wa Palestina."
Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kishia kutoka Iraq amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa, hasa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, yana jukumu la kimaadili na kibinadamu kuhakikisha kwamba janga hili haliruhusiwi kuendelea.
Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za dhati kukomesha maangamizi haya, na kuzitaka serikali za dunia kutumia kila mbinu inayowezekana kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na washirika wake, ili kuruhusu kuingizwa haraka iwezekanavyo chakula na bidhaa muhimu kwa raia wasio na hatia walioko Gaza.
Taarifa ya Ayatullah Sistani imekuja wakati ambapo baa la njaa linaendelea kutanda Gaza, huku mashirika ya kibinadamu yakionya juu ya ongezeko kubwa la utapiamlo na vifo vinavyohusiana na njaa kali.
Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa karibu watu nusu milioni wanakabiliwa na viwango vya juu kabisa vya njaa. Mashirika ya misaada yameripoti kuwa zaidi ya Wapalestina 100, watoto wakiwa ndio waathirika wakuu, wamefariki dunia kwa njaa katika wiki chache zilizopita, huku hospitali zikishindwa kutoa huduma kwa maelfu ya watoto waliokonda kupita kiasi.
Ufikishaji wa misaada ya kibinadamu bado unakumbwa na vikwazo vikubwa, kutokana na hatua za kijeshi za Israel zinazozuia au kushambulia misafara ya misaada inayojaribu kufika Gaza ya kaskazini na kati.
Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa wameeleza kuwa hali hiyo ni baa la njaa lililotengenezwa kwa makusudi na wameitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel mashinikizo ya moja kwa moja ili kuondoa mzingiro mara moja.
3493987