Barua hiyo, iliyoandikwa wakati ambapo maangamizi ya kibinadamu yanaendelea, inawaomba waqarii mashuhuri wa Misri kutumia nafasi yao kushawishi uungwaji mkono kwa watu wa Palestina walioko chini ya mzingiro.
Sehemu ya barua hiyo inasema:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mrehemevu
"Hakika hii Qur’ani inaongoza kwenye njia iliyo sawa kabisa." (Surah Al-Isra, aya ya 9)
Sisi, jamii ya waqarii wa Qur’ani Tukufu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tunaandika barua hii kwa huzuni na hisia kali ya kuwajibika kwa ajili ya Ummah wa Kiislamu, maumivu ya pamoja ambayo yamejeruhi nyoyo za kila muumini wa kweli na mpenda haki katika siku hizi ngumu.
Gaza leo ndiyo sehemu yenye majeraha makubwa zaidi ya Ummah, ikilia chini ya vifusi vya mzingiro na vita.
Watoto wanyonge, wanawake wanaokumbwa na njaa, na majeruhi wasiokuwa na dawa wala hifadhi—ndiyo taswira halisi ya Gaza kwa sasa.
Huu ndio wakati ambapo sauti ya Qur’ani inapaswa kusikika siyo tu kutoka kwenye vinywa vyetu bali pia kupitia msimamo wetu:
"Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako."
(Surah An-Nisa, aya ya 75)
Mojawapo ya njia muhimu za kuokoa Gaza ni kufungua kivuko cha Rafah—mshipa wa uhai ambao kufungwa kwake kumeizuia Gaza hata pumzi ya matumaini. Kupitia kivuko hiki, si chakula na dawa tu vitakavyopita, bali pia tumaini la maisha.
Nasi tunafahamu kwamba nyinyi, watu wa heshima wa Qur’ani wa Misri, mna nafasi ya kipekee katika dhamiri ya Ummah, taasisi za kidini, na hata katika maamuzi ya nchi yenu.
Tuisikie Qur’ani wakati huu kwa matendo, si kwa sauti tu—tusimame na wanyonge kwa ujasiri na imani.
Miongoni mwa waliotia sahihi barua hii ni:
Abbas Salimi, Ahmad Abolqassemi, Karim Mansouri, Mohammad Reza Pourzargari, Shahriar Parhizgar na Hamed Shakernejad—wote ni waqarii maarufu na wahifadhi wa Qur’ani kutoka Iran.
3494059