IQNA

Mahakama ya Uholanzi yasema upelelezi kuhusu Msikiti wa Veenendaal ulikiuka haki za Waislamu

7:43 - August 02, 2025
Habari ID: 3481030
IQNA – Mahakama moja nchini Uholanzi imebaini kuwa halmashauri ya jiji la Veenendaal ilifanya upelelezi kinyume cha sheria dhidi ya taasisi ya Kiislamu ya Taubah na msikiti wake bila ridhaa yao.

Mahakama ya Kiholanzi imetoa uamuzi kuwa halmashauri ya Veenendaal ilikiuka haki kwa kuamuru uchunguzi wa siri dhidi ya taasisi ya Taubah na msikiti wake, jambo lililokiuka haki ya faragha ya jamii ya Kiislamu. Uamuzi huu ni wa kwanza kutolewa kuhusu mfululizo wa uchunguzi unaolenga jamii za Kiislamu katika miji kadhaa ya Uholanzi, kama vile Almere na Delft.

Uchunguzi huo ulifanyika mwaka 2018 na uliendeshwa na kampuni binafsi ya NTA (Training & Advice), bila taasisi ya Taubah kufahamishwa hata kidogo.

Kwa mujibu wa matokeo ya mahakama, licha ya Veenendaal kudai kuwa baadhi ya waliohojiwa walifahamishwa, taasisi ya Taubah na wanajamii wake hawakushirikishwa, na taarifa za ndani zilikusanywa pasipo idhini. Mahakama ilihitimisha kuwa mchakato huo ulikosa uwazi na haukufuata viwango vya haki vinavyotakiwa kisheria.

Wakosoaji wamesema kuwa aina hii ya uchunguzi ni mfano wa ubaguzi wa kitaasisi na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia). Tabia ya kuajiri makampuni binafsi kuchunguza jamii za misikiti bila uangalizi wa serikali ilizua hofu kubwa ya kitaifa baada ya kufichuliwa na vyombo vya habari vya NRC na Bureau Spotlight mwaka 2021.

Barua pepe zilizovuja zilionyesha kuwa ripoti ya uchunguzi huo ilisambazwa kwa wizara mbalimbali za serikali pamoja na idara ya ujasusi ya AIVD, bila taasisi ya Taubah kupewa nafasi ya kujibu au kutoa maoni.

Halmashauri ya Veenendaal sasa inalazimika kisheria kufichua ni nani wote waliopokea ripoti hiyo ndani ya siku 30 au italazimika kulipa faini ya kila siku.

Mjumbe wa bodi ya Taubah, Bilal Riani, alikaribisha uamuzi huo akisema ni “wa kupendeza sana,” kwa mujibu wa gazeti la NL Times.

Meya wa Veenendaal, Gert-Jan Kats, alitoa msamaha wa hadharani, akikiri madhara yaliyosababishwa na kuahidi kushirikiana na jamii ya Kiislamu ili kujenga tena uaminifu.

3494069

captcha