Shirika hilo limesema litatumia uwezo wake wote kuhakikisha mpango wa ibada ya Arbaeen unatekelezwa kwa mafanikio. Msemaji wa Shirika la Mikingo ya Mpaka, Alaa al-Din al-Qaisi, alisema katika taarifa kwamba kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Iraq, Mheshimiwa Muhammad Shia al-Sudani, ya kutoa huduma bora kwa wafanyaziyara wa Arbaeen na kurahisisha uingiaji wao bila kucheleweshwa, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Omar Adnan al-Waeli, ameagiza wafanyakazi wote wa shirika kuwepo kazini kwa tahadhari ya hali ya juu na kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, na idara nyingine husika katika jambo hili.
Aliongeza kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya kuwapokea wafanyaziyara kupitia mipaka ya ardhini (Al-Mandhariyyah, Zarbatiyah, Al-Shayb na Shalamcheh), mipaka ya Serikali ya Kikanda ya Kurdistan ya Iraq (Bashmaq, Hajj Imran na Ibrahim Al-Khalil), na viwanja vya ndege vya kimataifa (Baghdad, Kirkuk na Basra).
Pia alisema kuwa mpango wa Shirika la Mikingo ya Mpaka unajumuisha uratibu na ofisi za mikoa zenye mipaka ya kuingilia ili kuandaa miundombinu muhimu katika maeneo wanayopita wafanyaziyara, na kurahisisha safari ya Arbaeen kuanzia mpakani hadi Karbala, pamoja na kuhakikisha kurejea kwao salama.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa hasa na Waislamu wa madhehebu ya Shia siku ya arobaini baada ya Ashura, likikumbuka kuuawa shahidi kwa Imamu Hussein (Alayhis Salaam), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye pia ni Imamu wa tatu wa Mashia.
Ni moja ya ibada kubwa zaidi duniani kwa mwaka, ikihudhuriwa na mamilioni ya Waislamu wa Shia, pamoja na masuni na hata wafuasi wa dini nyingine, wakitembea kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itaangukia tarehe 14 Agosti.
3494057