IQNA

Kundi la Kwanza la Wasomaji wa Msafara wa Qur'ani kutoka Iran Waanza Shughuli Zao Najaf

23:38 - August 06, 2025
Habari ID: 3481044
IQNA – Kundi la kwanza la wahudumu wa Qur'ani kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, walioko katika Msafara wa Qur'ani wa Arbaeen, wamewasili Iraq mapema wiki hii na wameanza kufanya shughuli mbalimbali za Qur'ani katika mji mtukufu wa Najaf.

Moja ya shughuli hizo ilifanyika katika Mawkib (kituo cha huduma kwa wafanyaziyara) kilichoandaliwa na Idara ya Wakfu na Hisani katika mkoa wa Qazvin katika Husseiniyah ya Ayatullah Shahroudi mjini Najaf.

Kundi hili litaendelea na shughuli zao za Qur'ani katika njia ya matembezi ya Arbaeen kuanzia Najaf hadi Karbala, na linatarajiwa kuwasili Karbala siku ya Alhamisi, tarehe 7 Agosti, kwa ajili ya kufanikisha shughuli yao ya mwisho.

Kundi hili lina jumla ya watu ishirini, wengi wao wakiwa ni vijana wasomaji wa Qur’ani kutoka Kikosi cha Kitaifa cha Oswah, ambao wamepelekwa Iraq kama kundi la kwanza la Msafara wa Qur’ani wa Arbaeen kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maarufu kama Msafara wa Qur’ani wa Imam Ridha (AS).

Awali, Sayyid Muhammad Mojani, kiongozi wa Kikosi cha Shughuli za Qur’ani cha Kamati ya Kiutamaduni ya Makao Makuu ya Arbaeen, alisema kuwa kulingana na mipango, wanachama wa msafara huo, zaidi ya wasomaji wa Qur’ani themanini pamoja na wahudumu wa shughuli za Qur’ani, wataelekea Iraq katikati ya mwezi wa Safar katika awamu nne tofauti.

Shughuli zao za Qur’ani zitaendelea katika mji mtukufu wa Karbala hadi Siku ya Arbaeen, na baada ya hapo wataanza kurejea nchini Iran.

Maombolezo ya Arbaeen, ambayo mwaka huu yataangukia tarehe 14 Agosti, ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani.

Siku hiyo huadhimisha siku ya arobaini tangu tukio la Ashura, siku ya kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imamu Hussein (AS).

Kila mwaka, maelfu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka mataifa mbalimbali, hasa Iraq na Iran, hujitokeza kwa wingi mjini Karbala, mahali alipozikwa Imamu Hussein (AS), kwa ajili ya kushiriki katika ibada na maombolezo.

Wafanyaziyara hao hutembea kwa miguu kutoka maeneo mbalimbali hadi Karbala kwa ajili ya kujipatia baraka na kujielekeza kwa Mwenyezi Mungu kwa namna ya kiroho.

Iran pia hutuma msafara wa Qur’ani, unaojulikana kama Msafara wa Nuru, kuelekea Iraq katika kipindi cha Arbaeen.

Wajumbe wa msafara huu hushiriki katika shughuli mbalimbali za kidini na Qur’ani kama vile usomaji wa Qur’ani Tukufu, kuitwa kwa adhana, na nyimbo za Tawasheeh (tenzi za kidini), hasa katika njia ya kutoka Najaf hadi Karbala na katika maeneo mengine ya matembezi ya Arbaeen.

Msafara wa mwaka huu unajulikana kwa jina la Msafara wa Imam Ridha (AS).

/3494144

 

Kishikizo: arbaeen QURANI TUKFU
captcha