IQNA

Benki ya Kiislamu Kushirikiana na Al-Azhar Kuandaa Mashindano ya Qur'ani

23:52 - August 06, 2025
Habari ID: 3481046
IQNA – Mashindano ya tatu ya kila mwaka ya kuhifadhi Qur’ani yanayoandaliwa na Msikiti Mkuu wa Al-Azhar nchini Misri yatafanyika kwa ushirikiano na benki ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa tovuti ya An-Naba, mashindano haya yatakuwa chini ya usimamizi wa Sheikh Ahmad Al-Tayyib, Imamu Mkuu wa Al-Azhar, kwa kushirikiana na Benki ya Kiislamu ya Faisal.

Sheikh Abdul Munim Fuad, ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Kielimu katika taasisi ya Al-Azhar, alisema kuwa mashindano haya yamepangwa kwa makundi tofauti ya umri, na wale wanaopenda kushiriki wanahimizwa kutembelea tovuti rasmi ya Al-Azhar kwa ajili ya kujisajili.

Ameeleza kuwa mashindano haya ni fursa adhimu kwa washiriki kupima uwezo wao wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu na kuimarisha umahiri wao katika masomo ya Qur’ani.

Kwa upande mwingine, Sheikh Hani Awdah, msimamizi wa Msikiti Mkuu wa Al-Azhar, alisema kuwa teknolojia ya sauti na video itatumika katika mchakato wa tathmini ya washiriki ili kuhakikisha uwazi na haki kwa wote.

Ameongeza kuwa zaidi ya pauni milioni moja na nusu za Kimisri zimetengwa kama zawadi kwa washindi bora kutoka katika makundi mbalimbali ya umri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashindano yatahusisha makundi yafuatayo:

  • Kuhifadhi Qur’ani yote kwa Tajweed kwa kundi la umri wa miaka 22 hadi 28

  • Kuhifadhi Qur’ani yote kwa Tajweed kwa walio chini ya miaka 15

  • Kuhifadhi thuluthi mbili (2/3) ya Qur’ani kwa walio chini ya miaka 12

  • Kuhifadhi thuluthi moja (1/3) ya Qur’ani kwa walio chini ya miaka 10

Usajili utaendelea kwa muda wa siku kumi kupitia tovuti rasmi ya Al-Azhar, na vituo vya mitihani vimewekwa katika mikoa mbalimbali ya Misri ili kurahisisha ushiriki wa mahafidhina kutoka maeneo yote ya nchi.

3494139/

Habari zinazohusiana
captcha