IQNA

Ahukumiwa mwaka mmoja jela kwa kuvunjia heshima nakala ya Qur'ani nchini Ufaransa

14:25 - August 01, 2025
Habari ID: 3481024
IQNA – Mwanaume mwenye umri wa miaka 27 nchini Ufaransa amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa kitendo cha kuvunjia heshima Qur'ani, Kitabu Kitakatifu cha Uislamu.

Mahakama ya Jinai ya Lyon ilimhukumu jamaa huyo siku ya Jumatano kwa kuhusika kwake na tukio la kuchoma nakala ya Qur’an Tukufu mnamo mwezi Juni nje ya msikiti wa Villeurbanne.

Mahakama pia imempiga marufuku ya kuingia katika mji wa Villeurbanne kwa kipindi cha miaka miwili.

Mtuhumiwa alichukua nakala ya Qur’an na kuichoma moto nje ya msikiti wa Errahma mjini Villeurbanne usiku wa kuamkia Juni 1 hadi 2, mwaka 2025.

Shahidi mmoja aliuzima moto huo na kuwataarifu viongozi wa msikiti siku iliyofuata.

Kamera ya ulinzi ilinasa tukio hilo la chuki dhidi ya Uislamu, jambo lililosaidia polisi kumkamata mtuhumiwa kwa haraka.

Mtuhumiwa alishtakiwa kwa kosa la “uharibifu uliotokana na chuki ya kikabila, kitaifa, au kidini.”

Ingawa hivyo, mtuhumiwa alikana kuhusika na kitendo hicho cha chuki dhidi ya Uislamu, akidai kuwa yeye ni “mhanga wa maradhi yake.”

Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu kuliko nchi nyingine yoyote ya Ulaya Magharibi, ambapo inakadiriwa kuwa Waislamu wapatao milioni sita wanaishi nchini humo.

/3494074

Kishikizo: ufaransa qurani tukufu
captcha