IQNA

Iraq yazina njama ya hujuma ya kigaidi ya Daesh dhidi ya wafanyaziyara wa Arbaeen

0:25 - August 09, 2025
Habari ID: 3481054
IQNA – Gavana wa mkoa wa Karbala, Iraq, ametangaza kufanikiwa kuvuruga njama ya kigaidi iliyolenga wafanyaziyara wa Arbaeen katika eneo lake.

Nasif Jassim al-Khattabi, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, alisema kuwa kikosi cha kijasusi cha Al-Suqur (Tai) katika mkoa wa Karbala, chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Mahakama ya Uchunguzi ya Karbala, kilitekeleza operesheni ya kijasusi kwa kiwango cha juu cha usiri na usahihi.

Matokeo yake, magaidi 22 walikamatwa wakiwa na mpango wa kufanya mashambulizi, ikiwemo kupanda mabomu kando ya barabara ya wafanyaziyara wa Arbaeen, kushambulia vikosi vya usalama na maandamano ya Husseini, pamoja na kujaribu kuwekea sumu maeneo ya mikusanyiko ya wafanyaziyara, hasa kusini mwa mkoa huo, alibainisha.

Miongoni mwa mashambulio yaliyotibuliwa kulikuwa na jaribio la kushambulia moja ya Husseiniyah (vituo vya kidini) vilivyoko katika njia kutoka Karbala hadi Najaf, lakini mpango huo ulifeli kutokana na ushirikiano kati ya taasisi za usalama na mahakama, aliongeza al-Khattabi.

Waliokamatwa walipatikana na vielelezo vilivyothibitisha nia zao za kigaidi, na walikiri mahakamani kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIL au ISIS), afisa huyo alisema.
Aidha, baadhi ya magaidi hao walikuwa na mawasiliano na wahusika wa kigeni, akiwemo mtu mmoja aliyekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na utawala wa Kizayuni.

Gavana wa Karbala alisifu mchango wa Mahakama ya Uchunguzi ya Karbala na kikosi cha kijasusi cha Al-Suqur kwa kufanikisha kuzuia shambulio hilo, akisisitiza kuwa juhudi za usalama zitaendelea kuhakikisha usalama wa wafanyaziyara na mazingira salama kwa Arbaeen na matukio mengine ya kidini.

Arbaeen ni tukio la kidini linaloenziwa na Waislamu wa Kishia siku ya arobaini baada ya Ashura, kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu wa Kishia.
Ni miongoni mwa hija kubwa zaidi duniani, ikiwakusanya mamilioni ya Mashia, pamoja na idadi kubwa ya Masunni na wafuasi wa dini nyingine, wanaotembea kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, Arbaeen itaadhimishwa tarehe 14 Agosti.

3494160

Kishikizo: arbaeen daesh iraq
captcha