Wawakilishi wa dini za mbinguni barani Ulaya jana Jumatatu walikutana huko Brussels Ubelgiji, kwa lengo la kuchunguza mgogoro wa kifedha na kiuchumi unaoendelea hivi sasa ulimwenguni na kutafuta njia za kidini za kukabiliana na mgogoro huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Kuwait KUNA, kikao hicho ambacho ni cha tano tokea mwaka 2005 kinawashirikisha wawakilsihi wa dini zilizotajwa kutoka jumuiya ya nchi za Umoja wa Ulaya. Shakib bin Makhluf, Mkuu wa Muungano wa Jumuiya za Kiislamu barani Ulaya Stephen Lo, Mkuu wa Makanisa ya Harlem nchini Uingereza na Gilles Bernheim, Kuhani Mkuu wa Ufaransa ni miongoni mwa washiriki wa kikao hicho. Jose Manuel Barroso, Mkuu wa Umoja wa Ulaya na Hans-Gert Pöttering, Spika wa Bunge la Ulaya ndio waliosimamia kikao hicho. Barroso amesema kuwa mgogoro wa hivi sasa wa kifedha duniani umethibitisha kwamba masuala ya maadili na thamani za kidini, ambazo zimekuwa zikitawala Umoja wa Ulaya katika kipind cha miaka 50 iliyopita, zinapasa kutumiwa katika kutatua mgogoro huo. Amesema kuwa, kama tunavyoshuhudia katika pembe mbalimbali za dunia, nchi zinazozingatia misingi na thamani za kidini zimenusurika na mgogoro huo. 403287