Kimsingi Qur'ani Tukufu inaunga mkono taalumu zote zinazomletea Muislamu maendeleo ya kijamii, ustawi wa kiuchumi na kijeshi ili kwa njia hiyo Waislamu wasidhalilishwe na mataifa mengine na kuweza kujilinda dhidi ya maadui wao.
Hayo yamesemwa na Ayatullah Sayyid Riyadh al-Hakim, mkuu wa taasisi ya utamaduni wa Kiislamu ya Hakim ambaye pia ni muhadhiri wa Kituo cha Elimu ya Dini cha mjini Qum. Amesema Qur'ani inawasihi Waislamu katika nyingi ya aya zake kutafuta elimu kuwasifu wasomi na kulaani vikali ujahili na upumbavu. Amechambua uhusiano uliopo kati ya Qur'ani na taaluma mbalimbali na kusema kwamba, kwa kutilia maanani uzingatia mkubwa wa Qur'ani kwa Waislamu na Uislamu, na uzito mkubwa ambao umetolewa na kitabu hicho kitakatifu kwa ulazima wa kutetea dini, roho na ardhi za Waislamu, ni wazi kuwa kitabu hicho kinaunga mkono taaluma na elimu yoyote ile inayowaletea Waislamu maendeleo ya kijamii, ustawi wa kiuchumi na kijeshi. Amesema, kwa upande mmoja, Qur'ani Tukufu ni chanzo cha baadhi ya taaluma kama vile tauhid, utume, fiqhi, akhlaqi na itikadi na kwa upande wa pili kuunga mkono na kuwahimiza Waislamu wafuatilie baadhi ya taaluma kama vile ujuzi wa lugha. Amesema, ili kufahamu na kuweza kufasiri vyema Qur'ani Tukufu, mfasiri wa kitabu hicho cha wahyi anapasa kusoma na kujifunza masomo mengi ya kimsingi kama vile sarufi, nahau na balagha. Huku akiashiria makosa ya wataalamu wa masuala ya nchi za Mashariki ya kutenganisha Qur'ani na mafundisho halisi ya Uislamu. AlHakim amesema kuwa hilo ni kosa kubwa lililofanywa na watu hao wanaodai kuwa ni wataalamu wa Uislamu. 324608