Sahifa hiyo ni mjumuiko wa hotuba, risala, mahojiano, fatwa , miongozo ya kidini na barua za Imam Khomeini (SA) kuhusu masuala mbali mbali ya kimaadili, kisiasa na kijamii. Mjumuiko huo umeibuka kuwa hitajio kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu katika zama hizi zaidi ya wakati wowote ule. Katika mahojiano na IQNA Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammad Moqaddam Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Tassisi ya Kukusanya na Kueneza Athari za Imam Khomeini (SA) amesema kuwa: "Wanaovutiwa na fikra za Imam Khomeini (SA) katika nchi za Kiarabu walilalamika kutokana na kutofasiriwa Sahifa ya Imam kwa lugha ya Kiarabu. Maulamaa na wasomi katika nchi za Kiarabu wanaoifahamu lugha ya Kifarsi kwa mara kadhaa walitangaza kuwa tayari kuifasiri athari hiyo yenye thamani ya Imam Khomeini (SA) kwa lugha ya Kiarabu".
Ameongeza kuwa baada ya jitihada za karibu miaka kumi, Jildi 22 za Sahifa ya Imam Khomeini (SA) iliyofasiriwa kwa lugha ya Kiarabu ilizinduliwa katika maonyesho ya kimataifa ya vitabu yanayoendelea mjini Tehran. Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammad Moqaddam ameongeza kuwa Sahifa ya Imam Khomeini (SA) imefasiriwa kwa Kiarabu kufuatia juhudi za wataalamu 40 wakiwemo Muni Masoud, mfasiri maarufu wa Lebanon, Ali Ganjian na Sadeq Khurshah ambao ni wahadhiri bingwa wa lugha na fasihi ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Allamah Tabatabai mjini Tehran. Hujjatul Islam wal Muslimin Moqaddam amedokeza kuwa Sahifa ya Imam Khomeini (SA) imefasiriwa pia kwa muhtasari kwa lugha za Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kituruki, Kikurdi, Kijerumani na lugha nyinginezo muhimu duniani. 403806